‘RAGE, Julio baibai, Rage Julio baibai’, ndivyo mashabiki wa Simba walivyokuwa wakiimba jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar wakati wakimpokea kocha wao mpya, Zdravok Logarusic.
Katika mapokezi hayo yaliyoshuhudiwa na Championi Jumatatu, Loga aliyetua na ndege ya Shirika la Ndege la Qatar saa 2:15 asubuhi, alipokewa na viongozi mbalimbali wa Simba wakiongozwa na kaimu makamu mwenyekiti wa timu hiyo, Swed Nkwabi na wajumbe wa kamati ya utendaji, Danny Manembe.
Mashabiki waliofika uwanjani hapo, walikuwa wakiimba nyimbo za kejeli kwa mwenyekiti wao aliyesimamishwa Ismail Rage na aliyekuwa kocha msaidizi, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Wakati wa mapokezi hayo, mashabiki wa Simba walionekana kupagawa na furaha baada ya kumuona kocha wao ambapo naye alionyesha kushtushwa na furaha ya mashabiki hao na kuamua kukumbatiana nao kwa furaha.
Mara baada ya kutoka uwanjani hapo, Loga alipelekwa makao makuu ya klabu hiyo mitaa wa Msimbazi, Kariakoo, ambapo nako alikutana na mamia ya mashabiki wa timu na kuwaambia amefurahishwa na mapokezi hayo, sasa wampe muda afanye mambo mawili katika timu hiyo bila kusema ni nini atakifanya kabla ya kupelekwa katika hoteli aliyofikia.
Baada ya kufika hotelini, Loga aliwashtua viongozi wa Simba baada ya kutaka kuanza kazi rasmi bila ya kusaini mkataba kwa kutaka apelekwe katika uwanja wa mazoezi ambapo alipelekwa katika Uwanja wa Kinesi na kusema atafurahi kama akitafutiwa uwanja mwingine mzuri kidogo.
“Huu hauna shida sana lakini kama nitapata mwingine mzuri kidogo itakuwa sawa, nataka kufanya kazi ya uhakika ili tuweze kufanya mambo ya uhakika kidogo,” alisema Loga na kuhakikishiwa na Nkwabi kuwa hilo litashughulikiwa haraka.
Loga baada ya kumaliza hilo, aliwataka viongozi hao kuhakikisha timu inakusanyika mapema kwa lengo la kuwahi mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga, itakayopigwa Desemba 21, akaomba atafutiwe mechi nne za haraka za kirafiki ambazo zitamuwezesha kuwaona nyota wote wa kikosi hicho.
“Hatuna muda wa kutosha, najua watu wanataka kuona tunafanikiwa katika mechi hiyo, sitafuata program niliyoipanga, badala yake nataka mnitafutie mechi nne za kirafiki ambazo tutacheza kila baada ya vipindi vitatu vya mazoezi,” alisema Loga.
Kocha huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya anatarajiwa kusaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo leo Jumatatu baada ya kumaliza kufanya mazungumzo na uongozi wa Simba jana jioni ambapo Mcroatia huyo ametamba kuhakikisha anarudisha heshima ya klabu hiyo kwa kuwapa kombe moja.
No comments:
Post a Comment