
MANCHESTER United jana ikiwa kwenye Uwanja wa White Hart Lane ilijikuta tena kwenye hali ngumu baada ya kubanwa na Tottenham Hotspur na kutoka sare ya mabao 2-2.
Mchezo huu ulikuwa muhimu kwa United kushinda kwa kuwa ungewasaidia kusogea hadi kwenye tano bora katika msimamo wa Ligi Kuu ya England.Sare hii inawafanya United kubaki kwenye nafasi ya nane katika ligi hiyo ikiwa na pointi 22 katika michezo 13.
Katika mchezo wa jana, Spurs ambao walionyesha kiwango cha juu, walikuwa wa kwanza kujipatia bao katika dakika ya 17 baada ya mabeki wa United kuzembea kumkaba Kyle Walker ambaye aliifungia timu yake bao safi.
United waliamka baada ya bao hilo na kulisakama lango la Spurs kama nyuki na walifanikiwa kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji Wayne Rooney aliyefunga kwa ufundi wa hali ya juu.
Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1 na kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikitaka kupata bao la mapema.
Mbrazil Sandro alifanikiwa kuwafungia Spurs bao safi la pili kwa shuti kali kutoka nje ya eneo la hatari katika dakika ya 54.
Bao hilo halikudumu kwa muda baada ya kipa wa Spurs Hugo Lloris, kumchezea madhambi mshambuliaji wa United Danny Welbeck, eneo la hatari na mwamuzi kuamuru penalti ambayo iliwekwa kimiani na Rooney na kufanya matokeo kuwa 2-2.
Hata hivyo, matokeo haya siyo mazuri pia kwa Spurs ambayo inashika nafasi ya tisa wakiwa wamejikusanyia pointi 21.
No comments:
Post a Comment