

Mshindi wa milioni 50 za EBSS 2013, Emmanuel Msuya akiwapungia mashabiki baada ya kutangazwa mshindi.
Stori: Waandishi WetuBWA’ MDOGO aliyesafirishwa kutoka Jiji la Miamba (The Rocky City) a.k.a Mwanza, alidhihirisha kwamba yeye ni funga kazi baada ya kung’ara zaidi na kufanikiwa kujimilikisha kitita cha shilingi milioni 50 ambazo ndiyo zawadi ya mshindi wa Shindano la Epiq Bongo Star Seach (EBSS) 2013.

Pamoja na harakati nyingi zinazofanywa kwa lengo la kuwaongezea wanawake uwezo lakini Amina Chibaba, Elizabeth Mwakijambile, Maina Thadei na Melisa John hawakuweza kufua dafu kishindo cha Emanuel ambaye aliwafunika wote kisha kuchukua milioni 50 zake na kuzificha kibindoni.
Ushindi huo ni ishara kwamba kibao kimewageukia washiriki wa kike kwani huu ni mwaka wa tatu mfululizo wanachukua wanaume tu.
SIRI YA USHINDI WA EMANUEL
Tathmini iliyofanywa na Ijumaa Wikienda katika fainali ya EBSS 2013, iliyofanyika Jumamosi iliyopita (Novemba 30) kwenye Ufukwe wa Escape One, Mikocheni, Dar es Salaam, imebaini siri kubwa ya ushindi wa Emanuel.
Kwa mujibu wa tathmini hiyo, sauti yake nzuri, utulivu, ubunifu wa kujua hadhira inataka nini na uchaguzi mzuri wa nyimbo ndiyo uliomfanya Emanuel kushinda taji hilo.
Kila Emanuel alipopanda jukwaani kushusha karata yake, aliwaamsha vitini mashabiki, hivyo kuwa mshiriki aliyeshangiliwa zaidi na kwa pointi hiyo, majaji walikosa namna ya kumnyima taji.
Nyimbo Haya Mapenzi wa Bendi ya Diamond Musica International, Kitambaa Cheupe wa mkongwe King Kikii na Maneno Maneno ulioimbwa na staa wa Bongo Fleva, Ben Pol, zilimng’arisha Emanuel kuliko hata wimbo wake Leo ambao ni karata aliyoingia nayo katika fainali hiyo.
Katika fainali hizo, timu ya wanahabari wetu, Musa Mateja, Erick Evarist, Imelda Mtema, Richard Bukos na Denis Mtima waliweka kambi ukumbini hapo na kuwasiliana na mkuu wao aliyekuwa Makao Makuu Bamaga-Mwenge, Dar ili kukuletea laivu kile kilichojiri usiku huo.
SAA 4:45 USIKU TOP FIVE YATAJWA
Mkuu: Erick naona shughuli imechelewa sana, kulikoni?
Erick: Mkuu si unawajua Wabongo walivyo wa ajabu? Ukimwambia mtu saa mbili atafika saa nne.
Mkuu: Nawajua, hawajui kuwa muda ni mali. Nipe kinachojiri hapo kwa sasa.
Erick: Kabla ya kutajwa kwa tano bora (top tive), Martin Kadinda, yule modo wa kiume alikuwa anazingua kwenye zulia jekundu kwa kutaka picha kama mvua.
Mkuu: Hebu nitajie hiyo top five!
Erick: Top five ni Amina Chibaba, Elizabeth Mwakijambile, Emanuel Msuya, Maina Thadei na Melisa John.
Mkuu: Ok, ngoja nimcheki Mateja ananibipu.
Mateja: Kiongozi utofauti uliopo ni kwamba baada ya Salama Jabir, mmoja wa majaji waliozoeleka kutoonekana, kuna sura mpya za Fareed Kubanda ‘Fid Q’ na Banana Zorro.
Mkuu: Ina maana Madam Rita na Master J hawapo?
Mateja: Wapo kiongozi wanasifiwa kwa kutupia pamba hatari ila Salama ndiyo hayupo.
Mkuu: Ok, ngoja nimcheki Imelda.
SAA 5:30 USIKU FID Q, BARNABA KUHESABU KURA
Imelda: Kiongozi nilichokipata ni kwamba kura zitahesabiwa na Salvado, Fid Q na Barnaba so hakuna longolongo, leo ni tofauti kabisa na miaka mingine.
Mkuu: Ok, tafuta matukio mengine nyuma ya pazia.
SAA 5: 45 USIKU WASHIRIKI STEJINI
Denis: Mkuu hadi muda huu tayari washiriki wanne, Amina Chibaba, Elizabeth Mwakijambile, Emanuel Msuya na Maina Thadei wameshapanda stejini na kupafomu nyimbo zao wenyewe.
Mkuu: Kwa mtazamo wako nani kafunika?
Denis: Huyu Maina amekata viuno hadi meza ndogo ya majaji wakapagawa. Nasikia watu wanapiga kelele kuwa mpinzani wa Snura kapatikana.
Mkuu: Tafuta matukio kwa wahudhuriaji na mastaa.
SAA 6: 00 USIKU MSHIRIKI WA MWISHO STEJINI
Erick: Mkuu tayari washiriki wote wameshafanya shoo za awali stejini ambapo Melisa ndiyo kafunga pazia.
Mkuu: Ok. Kingine?
Erick: Mkuu nyuma ya steji namuona Snura anamtabiria Maina kuwa atafika mbali na ndiye mrithi wake.
SAA 6: 05 USIKU YOUNG KILLER AFUNIKA
Mateja: Kiongozi hapa kuna bonge la shangwe kwa huyu dogo anayerap, Young Killer. Siyo siri kafunika vibaya.
Mkuu: Inaelekea huyo dogo ni noma. Mateja hebu nitafutie matukio kwa wahudhuriaji hasa mastaa.
SAA 7:00 USIKU WAWILI WATUPWA NJE
Imelda: Mkuu raundi ya pili ndiyo imemalizika sasa kinachofuata ni mchujo, naona washiriki wote matumbo joto.
Mkuu: Watatolewa wangapi? Au ndiyo mshindi anatangazwa?
Imelda: Hapana Mkuu, hapa kitakachotokea ni kwamba washiriki wawili watachujwa na kubakiza tatu bora.
Mkuu: Enhee hebu tujuze nani anatoka na nani anabaki.
Imelda: Mkuu! Mkuu! Unanisikia? Tayari mshiriki wa kwanza kuyaaga mashindano ameshatangazwa. Ni Amina Chibaba yaani watu wanamsikitikia mno.
Mkuu: Lakini huyo naona kama alistahili kutoka, umejua wanatumia vigezo gani?
Imelda: Mkuu wanasema kura za mashabiki ndiyo zinaamua nani atoke na nani abaki. Mkuu! Mkuu… mshiriki mwingine anatolewa. Ni Maina Thadei, watu ni kama hawaamini vile.
1:10 USIKU MAINA AWALIZA MASHABIKI UKUMBINI
Mkuu: Erick upo kimya sana, umeona nini kwa upande wako?
Erick: Mkuu huyu mshiriki aliyetoka mwishoni, wanamuita Maina Thadei amewaliza kinoma mashabiki wake.
Mkuu: Kivipi? Hebu fafanua?
Erick: Inavyoonesha watu walimpa nafasi kubwa ya kuondoka na milioni hamsini hasa kutokana na umahiri wake wa kuzungusha nyonga, sasa alipotolewa kuna mashabiki wanamwaga machozi wanasema ameonewa.
Mkuu: Watu hawajui kwamba kinachoangaliwa hapo siyo mauno bali ni uwezo wa kucheza na sauti? Ok endelea ngoja nimcheki Denis.
MSHIRIKI AANGUKA JUKWAANI
Denis: Mkuu! Mbona nakupigia simu yako inatumika? Kuna tukio hapa mpaka limepita.
Mkuu: Tuliza munkari Denis? Si unajua wote mnaripoti kwangu? Haya tujuze ni tukio gani?
Denis: Mkuu wakati jina la mshiriki wa pili likitajwa, huyu msanii wa kiume, Emanuel Msuya alianguka jukwaani kwa hofu akidhani ni yeye ametolewa.
Mkuu: Duh! Sasa mtoto wa kiume anakuwa na hofu hivyo? Vipi si ameinuka lakini au kapoteza fahamu?
Denis: Wenzake wamemsaidia kuinuka, wala hajapoteza fahamu, naona ni hofu tu inamsumbua. Mchakato unaendelea sasa ambapo washiriki watatu waliosalia wanaingia kwenye raundi nyingine.
Mkuu: Ok endeleeni na kazi.
MELISA ‘OUT’
Bukos: Mkuu, washiriki watatu walioingia tatu bora wamechujwa kwa mara nyingine ambapo huyu mdada bongebonge huyu ametolewa. Yaani mimi ningekuwa jaji huyu ningempa ushindi hata wa mezani.
Mkuu: Bukos hebu kuwa ‘serious’ basi, mshiriki bongebonge ndiyo nani?
Bukos: Samahani mkuu, ni huyu Melisa John, jina lake lilinitoka kidogo. Washiriki wawili waliobaki wameingia kwenye raundi ya mwisho.
MSHINDI AANGUKA TENA JUKWAANI
Baada ya kutangazwa mshindi, Emanuel alianguka tena jukwaani kama ilivyokuwa mara ya kwanza na kumwaga machozi ya furaha.
Hongera kwake aisee
ReplyDeleteDuuuuuh tugawane
ReplyDelete