Thursday, March 13, 2014

SERIKALI YAJIPANGA KUWA NA SERA YA FILAM

Serikali ya Tanzania imejipanga kuendeleza
kwa dhati TASNIA ya Filamu ili kuwa chanzo
kikubwa cha ajira kwa wasanii na pia
kuongeza uchumi wa nchi .
Ni dhahiri kuwa sekta ya filamu ni njia
madhubuti ya kutambulisha jamii
kiutamaduni, kisiasa na kijamii na pia
katika kukuza na kuongeza fursa za nchi
katika uwekezaji na utalii.
Filamu na Makala za Filamu zikitumika
vizuri zitaweza kuhamisha na kuondoa
tofauti mbalimbali zilizopo ndani ya jamii
na hivyo kuongeza umoja na mshikamano
baina ya watu wa makabila na watu wenye
asili mbalimbali , hivyo kuutambulisha
utamaduni wa Mtanzania.
Kazi na shughuli za Filamu nchini zimekuwa
zikisimamiwa na Sera ya Utamaduni ambayo
ilitayarishwa na kupitishwa mwaka 1997
pamoja na Sheria ya Filamu na Michezo ya
Kuigiza na 4 ya mwaka 1976.
Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1997
hadi mwaka 2013 kumekuwepo na maendeleo
makubwa katika Tasnia ya Filamu nchini
hivyo kuisababishia Sera ya Utamaduni ya
Mwaka 1997 kutokidhi baadhi ya mahitaji
ya tasnia ya filamu na kupelekea mahitaji
ya kurekebisha Sera ya Utamaduni kama
Sera mama na kutungwa kwa Sera ya
Filamu.
Mnamo Desemba 12 mwaka 2013, wadau
mbalimbali kutoka Wizara ya Habari , Vijana
Utamaduni na Michezo , Bodi ya Filamu,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi na Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi walishiriki katika
kikao cha wadau cha kujadili rasimu ya
awali ya Sera ya Filamu.
Wadau wengine ni Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii , Wizara ya Kazi na Ajira, BASATA,
Idara ya Sanaa na Sanaa za Maonyesho ,
Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, Mamlaka ya
Mapato Tanzania, Mtandao wa Muziki,
Swahili Films , ROSAF , TAPAF , Umoja wa
Mashirikiano wa Filamu, Filamu Cental ,
Chama cha Hakimiliki Tanzania, Shirikisho
la Sanaa za Maonyesho pamoja na G & S
Associates and Advocates.
Hata hivyo wadau ambao hawakushiriki
walipewa nafasi na Serikali kuwasilisha
maoni yao ambapo mwitiko umekuwa mzuri
na maoni yanaendelea kupokelewa ili
hatimaye kuwa na Sera bora na shirikishi .
Katika kikao hicho Rasimu ya awali ya Sera
ya Filamu iliwasilishwa kwa kuelezea historia
fupi ya filamu nchini, vikao vya wadau
vilivyofanyika vya mapendekezo ya kuwa na
Sera ya Filamu kati ya mwaka 2004 na 2013,
nyaraka kama Mpango Mkakati wa Bodi ya
Filamu unaoonyesha haja ya kuwa na Sera
ya filamu pamoja na kuelezea malengo
mahususi na matamko ya Sera mpya
inayopendekezwa kutungwa .
Aidha , wadau walijadili uzoefu wa nchi
nyingine kama Kenya, Nigeria, China,
Afrika Kusini , Marekani , Canada , India na
Uingereza na matokeo ya tafiti mbalimbali
zilizofanyika pamoja na Changamoto
zinazoikabili Tasnia ya Filamu nchini.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na
wadau ni pamoja na kuwa Sera itamke
uanzishwaji wa Chuo cha Taifa cha Filamu ,
Sera itamke kuwepo kwa Mfuko ambao
utasaidia katika kuimarisha Sekta ya
Filamu na Sanaa za maonyesho kwa ujumla,
Sera itoe tamko kuhusu kusimamia maadili
katika tasnia ya Filamu na kudhibiti
ukatili wa kijinsia katika tasnia ya Filamu.
Pia walipendekeza kuwa hoja na matamko
yawe na takwimu zaidi , Sera itamke namna
ya kumlinda msanii wa Tanzania ,
mzalishaji wa ndani na wawekezaji, pamoja
na kupiga vita udhalilishaji wa watoto wa
kike.
Kwa upande mwingine, wadau hao walitoa
pongezi kwa Wizara kwa kuandaa Rasimu ya
awali ya Sera ya Filamu iliyotokana na
maoni mbalimbali ya wadau , Sera ambayo
itaiwezesha Tasnia ya Filamu kupata
mwelekeo bayana na kukidhi matakwa ya
kila mdau katika tasnia ya filamu .
Wizara inapenda kuujulisha umma kuwa
imekua na inaendelea kushirikiana na
wadau wa Filamu kwa kila hatua ili
hatimaye ifanikishe azma ya kuwa na
nyaraka zote muhimu katika kuendeleza,
kusimamia , kuratibu na kukuza tasnia ya
filamu nchini.

No comments:

Post a Comment

.