Wednesday, December 4, 2013

DENTI AUAWA NA MPENZI WAKE


KIFO cha kikatili cha mwanafunzi aliyeuawa
siku chache baada ya kuhitimu kidato cha
nne katika Shule ya Sekondari Luguruni na
mkazi wa Kimara Golani, Dar , Sharifa Rajab
( 18) bado ni simanzi nzito katika familia
yake.
Marehemu Sharifa Rajab enzi za uhai wake .
Sharifa aliuawa kikatili Novemba 22, mwaka
huu, Kimara Golani jijini Dar na mtu
anayedaiwa ni mpenzi wake ajulikanaye kwa
jina la Abdul ( 22) ambaye ni dereva wa
bodaboda.
SIMULIZI YENYE MAJONZI
Akizungumza kwa masikitiko makubwa, baba
wa marehemu , Rajab Abdallah alisema siku
ya tukio asubuhi, yeye na mke wake wakiwa
kazini, Sharifa aliondoka nyumbani hapo bila
taarifa na kuwaacha wadogo zake tu .
“Tuliporudi jioni , mimi na mama yake tulianza
kuhangaika kumtafuta bila mafanikio . Mwisho
tuliamua kurudi kulala japokuwa usingizi
ulikataa . Unajua tena mtoto ni mtoto . Huwezi
kupata usingizi wakati mwanao hujui aliko .
“Tulipanga siku iliyofuata kwenda kutoa
taarifa polisi , lakini ilipofika saa kumi na
moja alfajiri , tuliletewa ujumbe kwamba kuna
mwili wa mwanamke umekutwa kwenye
chumba cha jirani .
“Ilikuwa vigumu kusema kwamba mwili huo
ni wa mtoto wetu Sharifa , tuliamini kifo kipo ,
lakini watakufa wengine si mtoto wetu
Sharifa .
“Hata hivyo , tulifunga safari kwenda
kuuangalia mwili huo . Sikuamini hata kidogo
nilipogundua kwamba ni mwanangu ndiye
alilala kitandani , amekufa kwa kuchomwa
kisu kooni na kwenye mbavu zote, kitanda
chote kilijaa damu . Sharifa alikuwa si Sharifa
tena bali marehemu Sharifa , ” machozi
yanamlengalenga.
Anaendelea: “Inaniuma sana ! Mbaya zaidi
nilijua chumba hicho ni cha kijana ambaye
ni dereva wa bodaboda, anaitwa Abdul .
Nikajiuliza ina maana alikuwa ni mpenzi
wake? Sikupata jibu. ”
TABIA YA MAREHEMU
Baba wa marehemu aliongeza kuwa , kwa
kipindi chote cha uhai, Sharifa hakuwahi
kuonesha dalili kwamba alikuwa katika
uhusiano wa kimapenzi , alikuwa ni msiri
sana.
MTUHUMIWA WA MAUAJI AACHA UJUMBE
Habari zaidi zilidai kuwa , baada ya
mtuhumiwa huyo kutekeleza mauaji ya binti
huyo aliacha ujumbe wa maandishi akisema
kuwa watu wasihangaike kumtafuta kwani na
yeye anakwenda kujiua .
Hata hivyo , mtuhumiwa hakwenda kujiua ,
badala yake alifika Kituo Kikuu cha Mabasi
ya Mikoani ( UBT ) kutafuta usafiri wa kurudi
kwao Tanga lakini alipokosa aliamua
kujisalimisha katika Kituo cha Polisi Ubungo
na kukiri kuua.
Mmoja wa viongozi wa serikali ya mtaa
( hakutaka kutaja jina lake ) alisema
mtuhumiwa huyo alipohojiwa polisi alisema
hajui kilichotokea , akaomba apewe nafasi
akamzike mpenzi wake huyo.
KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni,
ACP Camilius Wambura alithibitisha kutokea
kwa mauaji hayo ambapo alisema kwa
mujibu wa mtuhumiwa alifanya kitendo hicho
kutokana na wazazi wa msichana huyo
kukataa yeye asimuoe na tayari alikuwa na
mchumba mwingine .
Marehemu Sharifa alizikwa Novemba 24 ,
mwaka huu katika Makaburi ya Golani Nzasa,
Dar . Mungu ailaze roho yake mahali pema
peponi. Amina.

2 comments:

.