Sunday, December 8, 2013

Hakuna mahali pa kukanyaga’ msibani kwa Mandela


“Kweli tuna mengi ya kujifunza, inaonekana msiba
huu wa Mzee Mandela umewaunganisha zaidi
Waafrika Kusini, maana wote bila kujali rangi
wala kingine chochote, wanaonekana kuomboleza
kwa dhati kutoka mioyoni kabisa.”
Johannesburg. Makazi ya Rais wa Kwanza
mzalendo wa Afrika Kusini yaliyopo
katika Mtaa wa Laa namba 12, Houghton
ambako ndiko alikokuwa hadi
alipokutwa na mauti, ni kama
hapaingiliki kutokana na wingi wa watu,
magari na vyombo vya habari kutoka
sehemu mbalimbali duniani ambavyo
vimeweka kambi katika eneo hilo, usiku
na mchana kufuatilia safari ya mwisho
ya kiongozi huyo.
Anga la mtaa huo na sehemu za jirani,
limehanikizwa na sauti nyingi za
nyimbo zikiongozwa na Wimbo wa Taifa
wa Afrika Kusini ‘Nkosi Sikeleli
Afrika’ (Mungu Ibariki Afrika),
ukifuatiwa kwa zamu na nyimbo za
kidini na zile za asili ambazo zinasifu
ushujaa wa Mandela.
Katika lango la kuingia kwenye makazi
hayo ya Mandela, kuna maombolezo ya
aina yake kwani yameambatana na kitu
ambacho kwa macho kinaonekana kama
shamrashamra kwa nyimbo za sifa na
kufurahia kile Waafrika Kusini
wanachokiita kazi nzuri ya kutukuka ya
Mandela aliyoifanya katika umri wa
miaka 95 ya uhai wake.
Mwandishi wetui alitembelea makazi
hayo ya Mandela jana na kushuhudia
umati mkubwa wa watu wakifika nje ya
nyumba yake kwa ajili ya kuomboleza;
wakiweka mashada ya maua, mishumaa
na kadi zenye ujumbe wa pole kwa
familia yake.
Miongoni mwa waliokuwapo katika eneo
hilo ni Mtanzania, Christer Mwageni na
watoto wake; Sabina na Faraja.
Mwageni alisema: “Kwa jinsi hali ilivyo,
huwezi kukwepa kuwa mwombolezaji,
mimi na wanangu tulikuja hapa
kutembea tu kwa siku tatu hivi lakini
tumejikuta tukishiriki msiba na hata
kama tungekuwa hatutaki kushiriki,
uhalisia unatulazimisha”.
“Kweli tuna mengi ya kujifunza,
inaonekana msiba huu wa Mzee
Mandela umewaunganisha zaidi
Waafrika Kusini, maana wote bila kujali
rangi wala kingine chochote,
wanaonekana kuomboleza kwa dhati
kutoka mioyoni kabisa.”
Katika eneo hilo la Houghton, ulinzi
umeimarishwa na polisi wako kila kona
na wamekuwa wakiwaelekeza
waombolezaji na watu wengine njia
sahihi za kufuata hadi kuyafikia makazi
ya Mzee Mandela kutoka na barabara
nyingi za kuingia katika eneo kufungwa
na nyingine kugeuzwa maegesho ya
magari ya waombolezaji.
Kwa ujumla, pilikapilika ni nyingi, lakini
katika lango kuu la kuingia makazi ya
Mandela, ulinzi ni mkubwa na hakuna
anayeruhusiwa kulikaribia isipokuwa
wanafamilia, vingozi wa Serikali na
watu wengine wenye shughuli maalumu.
Soweto, Mandela Square
Hali kama hiyo ipo katika makazi yake
ya zamani Mtaa wa Vilakazi Na: 8115,
Orlando Magharibi, Soweto ambako
kuna pilikapilika nyingi zinazoyahusisha
makundi ya watu kutoka ndani na nje
ya Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment

.