Thursday, December 5, 2013

HUOGOPI SKENDO , HALAFU UNAJIITA STAA !


AUNT Ezekiel ni muigizaji wa filamu mwenye
jina kubwa , linaloenda sambamba na
muonekano wake wenye mvuto, hasa
anapovaa mavazi yake yanayoonyesha
baadhi ya sehemu muhimu za mwili wake.
Kwa wasiomfahamu vizuri, Aunt ni mtoto wa
mwanasoka mahiri wa zamani wa Simba na
Taifa Stars , marehemu Ezekiel Greyson,
maarufu zaidi kwa mashabiki wa kabumbu
kama Jujuman . Alitamba katika miaka ya
sabini na mwanzoni mwa themanini.
Ni mmoja wa wasichana waliofanikiwa
kupata majina makubwa, ingawa uwezo wake
kama muigizaji, bado haujakidhi viwango !
Hivi karibuni Aunt, mke wa mfanyabiashara
Sunday Demonte , kijana wa Kitanzania
anayefanyia shughuli zake Ughaibuni,
alinukuliwa na chombo kimoja cha habari
akisema kuwa haogopi kukutwa na skendo ,
kwani hilo ni jambo la kawaida .
“Mimi sijali, ninachoangalia ni kuingiza
kipato , mambo mengine shauri yao, kuna
watu wananichukia na kunitungia uongo ,
huwezi kupendwa na kila mtu, msanii ni kioo
cha jamii, lazima upate skendo ili uweze
kujirekebisha, ” Aunt alinukuliwa akiliambia
gazeti hilo.
Ninazifahamu kidogo kazi alizoshirikishwa,
nyingi kati ya hizo akicheza na marehemu
Steven Kanumba . Aina ya uigizaji wake
haubadiliki, ni Aunt yule yule anayependa
kuvaa nguo zenye kuonyesha nje sehemu
kubwa ya matiti yake , maungo yake na hata
mavazi yake mara zote ni yenye utata
mkubwa.
Muigizaji mzuri ni yule mwenye kubadilika .
Leo anaweza kucheza vizuri kama
changudoa , kesho yake akafiti kiufasaha
kabisa kama mtoto yatima anayeishi katika
umaskini mkubwa, kabla ya keshokutwa
kumkuta akiigiza vyema akiwa ni msomi
mwenye mafanikio makubwa kimaisha!
Sifa hizo Aunt Ezekiel , kama walivyo mastaa
wengi wa Tanzania katika filamu , hana . Ni
muigizaji wa kuigiza matanuzi, demu bomba
mwenye mitoko mingi , mikogo na mambo
kama hayo, ndiyo maana hata mavazi yake ,
uigizaji wake ni wa aina ileile katika filamu
zote alizocheza !
Anasema haogopi skendo , anajali kuingiza
kipato . Anahitimisha kwa kukiri kwamba
skendo ni jambo la kawaida kwa mastaa,
kwani kwa kutokea hivyo , ndipo wao hupata
nafasi ya kujirekebisha !
Hawa ndiyo aina ya wasanii tulio nao, wenye
wafuasi lukuki mtaani, wanaosimama na
kusema wazi kuwa hawaogopi skendo . Mtu
makini na hasa anayetakiwa kuwa mfano,
hawezi kuwa haogopi skendo !
Ndiyo maana kumbe kila siku tunasikia , mara
kapiga picha za nusu utupu na kuzitupia
katika mitandao ya kijamii ili watu waone
‘ figa ’ . Mara amepigana na mwenzake club
( bila chanzo hasa cha ugomvi kuelezwa ,
ingawa ni rahisi kuamini walikuwa
wakigombea bwana) .
Ninaheshimu maoni yake ya kutoogopa
skendo , lakini napingana naye kwa kauli
kuwa ni kawaida kwa mastaa kupata skendo .
Siyo kweli . Wapo mastaa wakubwa , tena
wale wanaojua kazi , lakini hawajawahi kuwa
mabingwa wa skendo .
Riyama Ally ni mmoja ya waigizaji ‘ wanaojua’
kwa levo za Bongo, lakini siwezi kumuweka
katika orodha ya wauza sura wanaotumia
tasnia kwa malengo yao binafsi.
Wasanii wetu wanaponzwa na uwezo wao
mdogo wa ubunifu , ndiyo maana bado
wanaamini katika skendo ili kuwaweka juu.
Mtu anajisikia vizuri akiandikwa gazetini, bila
kujali anaharibu vipi ‘ image’ yake kwa jamii.
Eti wanasingiziwa, hivi kuna mtu gani makini
anaweza kukubali kunyamaza gazeti
linapoandika uongo dhidi yake?
Kuna namna moja tu unayoweza
kuwazungumzia hawa mastaa wetu wa aina
hii , kwamba wanatengeneza skendo
makusudi ili wavutie macho na masikio ya
wahanga wa ngono !

1 comment:

  1. Hahaha mwandishi amepanic anajua asipoumia story hainogi hahaha

    ReplyDelete

.