Na. M . M . Mwanakijiji
Mpigania haki za weusi na alama kuu ya
udhalimu wa mfumo wa Ubaguzi wa Rangi
nchini Afrika ya Kusini Mzee Nelson ‘ Madiba ’
Mandela amefariki dunia baada yakuugua
kwa muda mrefu kufuatia maambukizi ya
mapafu kushindwa kutengemaa kwa muda
sasa . Mzee Mandela ambaye kwa miezi
kadhaa sasa amekuwa akisumbuliwa na
matatizo ya maambukizi kwenye mapafu
yake amefariki dunia nyumbani kwake
ambako alipelekewa toka hospitali ya Moyo
ya Mediclinic mjini Pretoria, chini Afrika ya
Kusini baada ya familia yake kuomba kufanya
hivyo .
Nelson Mandela akiwa na Walter Sisulu
gerezeni katika Kisiwa cha Robben , Cape
Town .
Mzee Mandela alipelekwa hospitali hiyo
Jumamosi ya tarehe 8 Juni ikiwa ni baada ya
kuanza tena kusumbuliwa na mapafu; miaka
ya themanini akiwa kifungoni Mandela alipata
ugonjwa wa Kifua Kifuu ( TB) kutokana na
kazi ngumu ya kupasua mawe kama sehemu
ya adhabu ya kifungo chake . Aliondoka
hospitali hapo Septemba 1, 2012 baada ya
familia kuomba hivyo na kuahidiwa huduma
nzuri ya kitabibu nyumbani . Wakati
anaondoka hospitali hali yake bado ilikuwa
ya utulivu kidogo lakini isiyo na mabadiliko
makubwa. Mipango ya mazishi ambayo
inatarajiwa kuvuta maelfu ya watu na mamia
ya viongozi wa kimataifa inatarajiwa
kutangazwa punde.
Bw. Mandela ( 95) alikuwa Rais wa kwanza
mweusi wa Afrika ya Kusini kufuatia
kutokomezwa kwa utawala wa ubaguzi wa
rangi uliofanywa na Makaburu kwa karibu
miaka 400 ambapo watu weupe walijipa haki
ya kuwatawala na kuwabagua watu weusi.
Kabla ya kuwa Rais wa Afrika ya Kusini Mzee
Mandela alitumikia kifungo cha miaka 27 jela
ambako pamoja na kazi ngumu aliendelea
kuongoza kundi la wapigania haki wengine
kudai usawa , utu , na umoja wa Waafrika ya
Kusini. Mandela alikuwa ni mfungwa maarufu
zaidi wa kisiasa duniani ambapo harakati za
kutaka afunguliwe zilipiganwa na
wanaharakati sehemu mbalimbali duniani
licha ya upinzani wa Serikali ya Afrika ya
Kusini na Baadhi ya Nchi za Kimagharibi
ambazo zilimuona Mandela kama Ghaidi na
mchochezi .
Maisha yake ya awali
Mzee Mandela alizaliwa Julai 18, 1918 katika
kijiji cha Mvezo mji mdogo wa Umtatu Jimbo
la Cape . Akiwa ni mmoja wa watoto wa
Mzee Gadla Henry Mphakanyiswa Nelson
Mandela alikulia kwa mamake – mke wa tatu
wa Mzee Gadla – katika kijiji cha Qunu
ambako pamoja na shughuli nyingine za
nyumbani alikuwa mvulana mchunga
ng’ ombe .
Baadaye alianza masomo ya shule ya msingi
na baadaye Sekondari ambapo aliamini kuwa
alikuwa anaandaliwa kwa ajili ya utumishi
katika nyumba ya Chifu wa Kabila lake la
Xhosa kama mshauri. Hata hivyo baada ya
kurudi nyumbani kutoka masomoni mwaka
1940 alikuta kuwa Chifu Jongintaba
ameandaa ndoa Nelson Mandela pamoja
mtoto wa kiume wa Chifu huyo aitwaye
Justice walitoroka nyumbani na kwenda
kwenye Jiji la Johannesburg . Alifanya kazi
kama mlinzi katika Kampuni ya Madini ya
Crown lakini alifukuzwa kazi na msimamizi
wa pale baada ya kugunduliwa kuwa alikuwa
ametoroka kwao .
Mandela akiwa amevaa mavazi ya kabila
lake la Xhosa; alitoka katika familia ya
kichifu .
Kuingia Katika Siasa
Alipokuwa akiishi kwa muda na mmoja wa
binamu zake Nelson Mandela alitambulishwa
kwa mwanaharakati wa chama cha ANC Bw.
Walter Sisulu ambaye baadaye walifungwa
pamoja – Sisulu akitumikia miaka 25 jela .
Walter Sisulu alimtafutia kazi ya ukarani
katika kampuni ya Wanasheria ya Witkin ,
Sidelsky and Edelman. Akiwa hapo alifanya
masomo ya elimu kwa njia ya Posta ambapo
alikuwa anatafuta shahada yake ya kwanza.
Mwaka 1943 alihitimu masomo yake ya
sheria na kuanza kazi kama Mwanasheria
badala ya kurudi kijijini kutumika kwa Chifu .
Akiwa ameanza kazi kama Mwanasheria
Mandela aliendelea kuwa chini ya uangalizi
wa Walter Sisulu ambaye alikuwa
anaendeleza harakati za kudai haki za weusi.
Akikutana mara kwa mara na wanaharakati
wengine nyumbani kwa Sisulu Mandela
alikutana tena na rafiki yake Oliver Tambo .
Ilikuwa ni katika mikutano hiyo alikutana na
mwanamama Evelyn Mase ambaye walianza
uhusiano wa mapenzi na baadaye kufunga
ndoa yake ya kwanza Oktoba , 1944 .
Walijaliwa watoto wawili wa kiume na wa
kike; wa kiume Madiba “Thembi ” Thembikile
alizaliwa Februari 1946 na wa kike Makaziwe
alizaliwa mwaka uliofuatia lakini alifariki
miezi tisa baadaye baada ya kupata
maambukizi ya ugonjwa uti wa mgongo.
Mandela na mtoto wake wa kwanza wa
kiume Themi .
Baada ya uchaguzi wa 1948 ambapo watu
weupe peke yao walishirikia vyama vya
Herenigle Nacionale Party na Afrikaner Party
viliungana na kuunda chama cha National
Party ambacho kilikuwa na sera ya wazi ya
ubaguzi na kikapisha na kupanua ukali wa
sera ya ubaguzi kupitia sheria mbalimbali za
ubaguzi wa rangi . Serikali ya Kikaburu ikaja
na mojawapo ya Sheria kali kabisa za
kupambana na wanaharakati ambayo
inajulikana kama Ukandamizaji wa
Ukomunisti ya 1950. Sheria hii ilikuwa
inashughulikia karibu mambo yote
yanayohusiana na kuipinga serikali na
ikiwahusu watu wote. Migongano kati ya
ANC na Serikali ya Kikaburu ilianza kupamba
moto.
Mwaka 1952 Nelson Mandela alikamatwa na
utawala wa Makaburu kwa kile kilichodaiwa
kujihusisha na vitendo vya Kikomunisti chini
ya ile sheria iliyopitishwa miaka michache
nyume. Alihukumiwa miezi tisa jela na “kazi
ngumu ” lakini utekelezaji wa hukumu hiyo
ulisitishwa kwa miaka miwili . Lakini mwezi
Disemba mwaka huo huo Mandela alipigwa
marufuku kuzungumza na zaidi ya mtu
mmoja kwa miezi sita . Akiwa kiongozi wa
ANC hii ilimaanisha kuwa asingeweza
kufanya mikutano na wanachama wake.
Mwaka 1953 Mandela na rafiki yake Oliver
Tambo walifungua kampuni yao ya
Wanasheria katika Jiji la Johannesburg na
kuifanya kuwa kampuni ya kwanza ya
Wanasheria Weusi katika Afrika ya Kusini.
Walijishughulisha na malalamiko mbalimbali
ya wananchi hasa yanayohusiana na ukatili
wa kisiasa . Hata hivyo serikali ikitumia sheria
nyingine ikalazimisha kufungwa kwa ofisi
hiyo iliyokuwa na wateja wengi na
kuihamisha sehemu nyingine ambapo ilikuwa
ni vigumu kwa wateja kuifikia . Mwaka 1955
Mandela na wenzake walishirikiana kuandaa
kongamano kubwa la watu wa Afrika Kusini
ambao wanaamini katika taifa moja la watu
wamoja japo wanatoka katika makabila na
rangi mbalimbali . Katika kongamano hili
kulisainiwa kile kinachoaminika kama
mojawapo ya nyaraka muhimu kabisa za
kutetea usawa na utu wa watu wote ambayo
ilijulikana kama Freedom Charter .
Kufananisha hii ni sawasawa na Azimio la
Uhuru la Marekani au ile nyaraka ya
Waingereza ya Magna Carta. Kwa Tanzania
tunaweza kufananisha kabisa na Azimio la
Arusha. Freedom Charter ilitengeneza ramani
ya kujenga taifa la watu walio huru na sawa
katika Afrika Kusini.
Nelson Mandela na Oliver Tambo –
wanasheria .
Marafiki wawili – miaka mingi toka Kisiwa
cha Robben.
Hata hivyo kwa upande wa familia ndoa yake
kwa Evelyn ilianza kuwa matatani. Kulikuwa
na tuhuma za kukosa uaminifu ambapo
alidaiwa kuwa na mahusiano ya mapenzi na
baadhi ya kina dada wa ANC . Evelyn alijaribu
watengane lakini pamoja na jitihahada
mbalimbali za kupatana Nelson Mandela
aliamua kupeana talaka na mke wake wa
kwanza mwezi Machi 1958. Walikuwa
wamejaliwa mtoto mwingine wa kike. Wakati
huo wa mchakato wa talaka Nelson Mandela
alikuwa ameanza mahusiano na Winnie
Madikizela mmoja wa wafanyakazi wa
mambo ya kijamii . Walifunga ndoa Mwezi
Juni 1958 .
Ndoa ya Madiba na Winnie .
Migogoro na utawala wa kikaburu
haikukoma. Na Mandela alizidi kuwa na siasa
za mrengo wa kushoto . Njia za amani za
kupata mabadiliko ya kisiasa zilionekana
kutozaa matunda ; Mandela na wenzake
walianza kuamini katika njia za kimapinduzi
na za kutumia silaha . Hili lilimletea matatizo
zaidi na watawala wa Kikaburu . Hatimaye
Augusti 2, 1962 Nelson Mandela alikamatwa
na utawala wa Makaburu na kushtakiwa kwa
kuchochea mgomo wa wafanyakazi na
kuondoka nchini bila kibali . Mandela
alijiwakilishi mwenyewe mbele ya mahakama
huku akitumia nafasi hiyo kutoa hutuba
motomoto za kisiasa dhidi ya utawala wa
kibaguzi wa makaburu. Alikutwa na hatia na
kuamuriwa kufungwa miaka mitano jela ;
wakati anatoka mahakamani mashabiki wake
walisimama pembeni na kuimba wimbo wa
Mungu Ibariki Afrika ( Nkosi Sikeleli Afrika) .
Kesi ya Rivonia
Matatizo yake hayakufikia mwisho . Julai 11,
1963 polisi walivamia shamba la Lilliesleaf –
mji mdogo wa Rivonia nje ya Johannesburg)
ambapo pamoja na vitu mbalimbali waliamini
walikuta ushahidi wa kutosha kumhusisha
Mandela na mipango ya kuipindua serikali .
Mandela na wenzake walitumia shamba hili
kama sehemu yao ya kujificha huku Mandela
akijifanya ni mtunza bustani . Kesi hii ilikuwa
motomoto kwani Mandela na wenzake
walishtakiwa kwa makosa manne yakiwa ni
ya uhujumu wa miundo mbinu ya nchi
( vitendo zaidi ya 200 ) pamoja na kutaka
kupindua serikali ; serikali ilikuwa
inapendekeza kuwa wakikutwa na hatia basi
wahukumiwe kifo. Mashahidi wengi wa
serikali waliitwa pamoja na lundo la ushahidi
wa picha na nyaraka kuthibitisha mashtaka
ya serikali dhidi ya Mandela na
wenzake tisa .
Mara baada ya kuachiliwa mwaka 1990
Mandela alihakikisha anamtembelea rafiki
yake mpenzi Oliver Tambo aliyekuwa
anapata matibabu Sweden.
Wengine ambao walikuwa pamoja na
Mandela ni pamoja na Walter Sisulu na
Govan Mbeki ( baba yake na Thabo Mbeki
aliyemrithi Mandela kama Rais wa Afrika ya
Kusini) . Ilikuwa ni katika kesi hii ambapo
Mandela alitoa mojawapo ya hotuba
zinazosifiwa zaidi duniani na ambayo
inasomwa na wanafunzi wa siasa sehemu
mbalimbali duniani kwani ilielezea falsafa ya
kupinga ubaguzi wa rangi . Inafanana sana
kimaudhui na barua ya Martin Luther King Jr
akiwa katika jela ya Birmingham huko
Alabama ambapo alielezea kwanini alikuwa
anapinga kubaguliwa na kwanini kila mpenda
haki duniani anapaswa kufanya hivyo hivyo .
Katika hotuba hii inayojulikana kama “I ’ m
Prepared to Die Speech” Mandela alisema
kuwa alikuwa anapigania haki ya watu weusi
kuheshimiwa kutokana na utu wao na kuwa
wao ni sawa kama binadamu wengine.
Alisema kuwa hapiganii haki ya weusi
kuwabagua weupe bali haki ya watu wote
kuishi kwa pamoja kama watu wa jamii
moja. Mandela alisema “This is the struggle
of the African people , inspired by their own
suffering and experience . It is a struggle for
the right to live . I have cherished the ideal of
a democratic and free society , in which all
persons live together in harmony and with
equal opportunity. It is an ideal which I hope
to live for and achieve . But , if needs be , my
Lord, it is an ideal for which I am prepared to
die ”. Yaani , “Haya ni mapambano ya watu
wa Afrika yaliyotokana na mateso na
mang ’ amuzi yao wenyewe . Haya ni
mapambano ya kupigania haki ya kuishi .
Nimelifurahia wazo la jamii ya kidemokrasia
na huru, ambapo watu wote wanaishi katika
amani na haki sawa . Ni wazo ambalo
ninatumaini kuishi kwa ajili yake na
kulitimiza. Lakini , ikibidi , mheshimiwa, ni
wazo ambalo nimejiandaa kufa kwa ajili
yake”.
Baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha
Mandela na wenzake wakitoka Mahakamani .
Pamoja na utetezi wake wote timu ya
Mandela ilishindwa kesi hii na wote
wakakutwa na hatia isipokuwa mmoja . Kwa
vile tayari kulikuwa na mwamko sehemu
mbalimbali duniani kupinga adhabu ya kifo
Mahakama ikawaamuru Mandela na wenzake
kutumikia kifungo cha maisha na huo ndio
ukawa mwanzo wa kifungo cha karibu miaka
30 jela ( ikumbukwe kesi hii ilipoanza Mandela
tayari alikuwa anatumikia ile hukumu ya
miaka 5 jela ) . Mandela na wenzake
walipelekwa katika jela ya Kisiwa cha Robben
ambako pale peke yake alitumikia miaka 18 .
Maisha kifungoni Kisiwa cha Robben na
kwingine .
Kisiwa cha Robben ambako Mandela
alifungwa kwa miaka 18 .
Mandela na wenzake walihukumiwa kazi
ngumu vile vile na kweli ilikuwa ni kazi
ngumu kwani pamoja na kuponda mawe
walipewa baadaye kazi ya kuponda mawe ya
chokaa. Kwa muda alikatazwa kuvaa miwani
ya jua kitua mbacho kilimsababishia ubovu
wa macho ambao hakuweza kupona kabisa .
Akiwa kifungoni mamake alimtembelea
mwaka 1968 na siku chache baadaye alifariki
dunia, mwaka uliofuata mtoto wake wa
kwanza Thembi alifariki katika ajali ya gari –
Mandela hakuruhiswa kuhudhuria mazishi
yao wote hao. Maisha kifungoni yalikuwa
magumu kwa kila kipimo licha ya maisha
baada ya miaka kuanza kuboreshwa kidogo
kufuatia maandamano na harakati za kutaka
Mandela afunguliwe. Utawala wa makaburu
hawakusikia la mtu yeyote hasa kwa vile
walikuwa wanaushirika wa karibu na serikali
ya Marekani na Uingereza ambazo zote
zilimuona Mandela kama Mkomunisti na
Ghaidi.
Mwaka 1966 gerezani Mandela anaonekana
akiitia viraka nguo yake ya jela .
Mandela alitumikia pia katika magereza ya
Pollsmoor huko Cape Town na Gereza kati ya
1982 hadi 1988 na baadaye gereza la Victor
Verster 1988 -1990 ambako kwa kiasi
kikubwa alikuwa amepewa maisha ya unafuu
( hapa chini akiwa na mpishi na huduma
mbalimbali ) kulinganisha na alivyoishi katika
gereza la Kisiwa cha Robben.
Akiwa gereza la Victor Verster alipewa
nyumba na mtumishi . Hapa pichani na
aliyekuwa mpishi wake kwenye gereza hilo .
Ikumbukwe miaka aliyokuwa Robben ndiyo
ilikuwa migumu zaidi kwani hakuruhusiwa
kutembelewa na watu wengi na alipewa
nafasi ya kutembelewa na kuandikwa barua
moja tu kila baada ya miezi sita . Katika
magereza hayo mengine Mandela alipata
unafuu kidogo .
Kuingia kwa F. W. de Clerk na kuachiliwa
kwa Mandela
Chini ya utawala wa Pieter Botha Afrika ya
Kusini ilizama katika siasa na sera za
ubaguzi wa rangi . Botha aliwachukia weusi
na aliamini kabisa kuwa utawala wa kikaburu
utadumu kwa muda mrefu. Botha anaweza
kabisa kufananishwa na aliyekuwa Gavana
wa Alabama George Wallace ambaye aliapa
kuwa “ubaguzi sasa , ubaguzi kesho , ubaguzi
milele”; japo aliishi na kuona Ubaguzi
ukifumuliwa katika jimbo lake na katika
Marekani sera hizo zikitupwa katika mifumo
ya utawala . Hata hivyo alikuwa ni F. W. de
Clerk mwanasiasa mwingine mzungu ambaye
licha ya kutoka katika chama kilichoamini
katika ubaguzi wa rangi yeye mwenyewe
alijikuta akiukataa kifikra kwani aliona
hauwezi kudumu .
Kwa muda hivi tangu 1988 Mandela alikuwa
na mazungumzo ya siri na baadhi ya
viongozi wa serikali juu ya masharti ya yeye
na wenzake kuachiwa huru na mwelekeo wa
siasa za Afrika ya Kusini . Mazungumzo hayo
yalikumbana na vikwazo vingi sana ikiwemo
kutokukubaliana kwa masharti – kwa mfano
serikali ilitaka Mandela asijiingize kwenye
siasa na kuwa wasilazimishwe kuwa na
utawala wa wengi ( majority rule) masharti
ambaye Mandela aliyakataa.
Baada ya Mdahalo mzito ambao de Klerk
alionekana kushinda ; Mandela alipompa
mkono alionekana kushangaza umati wa
watu na kujenga daraja kati yake na de Klerk
kwa maisha .
Matokeo yake ni kuwa Mandela na wenzake
waliachiliwa huru na utawala lwa De Clerk
Februari 2, 1990 na kuleta furaha
wanaharakati pote duniani . Ikumbukwe kwa
Tanzania wimbo maarufu wa “Kilicho cha
Wapenda Haki Duniani Kote” ulivuma sana
wakati huo katika kuhamasisha Mandela na
wenzake waachiliwe huru. Baada ya
kuachiliwa huru muda mrefu ulitumika
kufanya mazungumzo na utawala wa
kikaburu kuhusiana na mwelekeo wa siasa za
Afrika ya Kusini na hata kuelekea uchaguzi
mkuu. Hata hivyo kutokana na matukio
mbalimbali ya vurugu na mauaji ya kisiasa
yaliyokuwa yanaendelea na hata migongano
ya chama cha Inkatha cha Chifu Buthelezi
Mandela aliona hana jinsi isipokuwa kufikia
makubaliano ya msingi. Baadhi ya
makubaliano hayo yalihusisha kufunguliwa
kwa wafungwa wa kisiasa, kuitishwa kwa
uchaguzi mkuu , kuwa na Katiba ya Mpito na
kuhakikishia kuwa kazi za weupe
hazitafukuzwa kama ukiingia utawala wa
weusi.Mandela na de Klerk walitunukiwa tuzo
ya Nishani ya Amani ya Nobel mwaka 1993
Mandela na de Klerk wakionesha nishani ya
Nobel
Uchaguzi Mkuu wa 1994
Hatimaye Afrika ya Kusini ikaingia katika
uchaguzi mkuu wa kwanza huru na
wawananchi wote mwaka 1994 , Aprili 27.
Kampeni ilikuwa na vurugu za hapa na pale
lakini kwa ujumla wananchi wa Afrika ya
Kusini hasa weusi walijikuta kwa mara ya
kwanza wanapiga kura kumchagua kiongozi
wanayemtaka. Mandela akiongoza ANC
walishinda asilimia 62 ya kura na kushindwa
kupata theluthi mbili ambayo ingewawezesha
kuweza kubadili Katiba . Serikali yake ilikuwa
ni ya umoja wa kitaifa ikitegemea kwa kiasi
kikubwa baadhi ya maofis waliokuwa katika
utawala wa kikaburu. De Clerk alikuwa
Makamu wa kwanza wa Rais na Thabo
Mbeki akiwa Makamu wa Pili wa Rais .
Mandela ( katikati ) akiwa na Makamu wake
wawili
Mandela alishaeleza toka awali kuwa
atagombea kipindi kimoja tu na ndivyo
alivyofanya na baadaye kumwachia Thabo
Mbeki kama Rais wa Afrika ya Kusini. Baada
ya kustaafu siasa Mandela aliamua
kujishughulisha na program mbalimbali za
ndani ya Afrika ya Kusini na kutembelea
baadhi ya nchi . Hata hivyo udhaifu wa mwili
uliotokana na magonjwa na uzee ulimzidia na
kumfanya apunguze safari za nje . Kwa mara
ya mwisho alionekana katika shughuli za
hadhara katika mashindano ya Kombe la
Dunia mwaka 2010 ambayo yalifanyika Nchini
Afrika ya Kusini.
Mandela na Tanzania
Tanzania kama nchi imehusika kwa kiasi
kikubwa sana katika kuuvunja vunja utawala
wa kikaburu na katiak kuongoza harakati za
kutaka Mandela aachiliwe huru. Baba wa
Taifa Mwalimu Nyerere na utawala wake
mara baada ya Uhuru 1961 aliazimia kutoa
msaada wote unaohitajika kwa wapigania
uhuru wa Afrika ya Kusini . Kama
ilivyodokezwa hapo juu kuwa mojawapo ya
mashtaka dhidi ya Mandela ni lile la kwenda
nje ya Afrika ya Kusini bila kibali . Mwaka
1962 Mandela akitumia njia za panya
alitoroka Afrika ya Kusini na hatimaye kuingia
Tanganyika na kukutana na Mwalimu Nyerere
ambaye aliwapa ahadi ya ushirikiano
mkubwa. Mandela mwenyewe akizungumza
katika dhifa aliyomwandaliwa Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere mwaka 1997 Oktoba 17;
alisema “Inanyenyekesha kukumbuka
mchango wa Mwalimu Nyerere katika
ukombozi wa bara letu na Uhuru wa Afrika ya
Kusini”.
Aliendelea na kumsifia Nyerere kwa kusema
kuwa wakati watu wengine walikuja baadaye
kuona ubaya wa utawala kikaburu Nyerere
aliliona hili mwaka 1959 ambapo akishirikiana
na Fr . Huddleston walianzisha harakati za
kupinga ubaguzi wa rangi ( anti -apartheid
movement ) ambao zilikuja kuwa maarufu
sana baadaye – hasa baada ya kesi ya
Rivonia . Mandela alisema kukutana na
Mwalimu mwaka 1962 kulimuonesha jinsi
Nyerere alivyokuwa anataka haki sehemu
zote duniani na jinsi alivyojitoa yeye na taifa
lake changa kuona kuwa Afrika yote inakuwa
huru.
Wanaharakati – wakisherehekea miaka 80
ya Askofu Trevol Huddleston , Nyerere ,
Askofu Mkuu Desmond Tutu na aliyekuwa
Katibu wa Jumuiya ya Madola Shirdath
Ramphal.
Katika kuonesha hili Mandela alichagua
Tanzania miongoni mwa nchi za kwanza
kutembelea mara baada ya kuachiliwa huru
mwaka 1990 . Aliingia nchini Machi 7, 1990
na kupokelewa na maelfu ya watu
wakiongozwa na baba wa Taifa Mwalimu
Julius Nyerere pamoja na Rais Ali Hassan
Mwinyi . Wakati anatembelea nchini kama
mtu huru Tanzania ilikuwa na wapiganaji
karibu 10, 000 wa Afrika ya Kusini waliokuwa
wanaishi Tanzania na kujihusisha na mambo
mbalimbali . Ikumbukwe ANC ilifungua ofisi
yake ya kwanza nje ya Afrika ya Kusini Jijini
Dar -es - Saalam mwaka 1961 na hii ilichangia
baadaye pia kwa ofisi za vyama vingine vya
ukombozi kuchagua Dar kama makao yao
makuu.
Yote haya yalisaidia kuifanya Tanzania kuwa
makao makuu ya Kamati ya Ukombozi ya
Nchi Zilizo Mstari wa Mbele ambayo kwa
muda mrefu iliongozwa na Brig. Hashim
Mbita. Uhusiano huu wa karibu wa Tanzania
na Wapigania Uhuru ulithibitika zaidi baada
ya Tanzania kuwapatia wapigania uhuru hao
maeneo ya mafunzo ya kijeshi na taaluma
mbalimbali huko Morogoro eneo la Mazimbu
na maeneo mengine Mtwara na sehemu
nyingine nchini . Pamoja na vyuo wapigania
uhuru hao walipewa maeneo ya shule za
msingi na sekondari vile vile.
Wakufunzi wa chuo cha ANC Mazimbu
Morogoro enzi hizo.
Uhusiano huu wa karibu wa Tanzania na
wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini
ulionekana pia wakati wa Mkutano wa
Mawaziri Wakuu wa Nchi za Jumuiya za
Madola uliofanyika London , Uingereza .
Katika makala yake aliyoandika kwenye
gazeti la The Observer Machi 7 , 1961 Nyerere
aliweka msimamo wa Tanganyika mapema
kabisa kuhusiana na uanachama wa Afrika ya
Kusini kwenye Jumuiya hiyo ( Afrika ya Kusini
iliomba kuwa mwanachama na mawaziri
wakuu walitakiwa kuchukua uamuzi ) . Katika
makala hiyo Nyerere alisema mojawapo ya
mistari inayokumbukwa sana kuwa “kuipigia
kura Afrika Kusini ijiunge ni kutupigia kura
sisi kujitoa ( To vote South Africa in, is to
vote us out ) na inaaminikuwa kuwa hoja
aliyoijenga ilichangia sana kubadili upepo na
kusababisha Afrika ya Kusini kutoa ombi lake
la kujiunga. Uhusiano wa karibu wa Nyerere
na Mandela haukushia wakati huo tu ; hata
baada ya kifo cha Mwalimu alikuwa ni Nelson
Mandela aliyechukua jukumu la kusaidia
kuleta amani Rwanda kama Mpatanishi.
Buriani.
Mandela ametutoka baada ya maisha
ambayo ametumikia nchi yake , bara lake na
dunia kwa namna ambayo ameacha alama
ya kudumu ya kukumbukwa . Kwa mtu
ambaye utawala wa kikaburu ulimnyima haki
nyingi za msingi na kumchukulia miaka
ishirini na saba ya maisha yake angeweza
kuwa mtu mwenye kisasi pale aliposhika
madaraka kama Rais wa nchi yake . Mtu
ambaye alinyanyaswa , kuteswa , na
kushindwa hata kuhudhuria mazishi ya
mamake kwa namna ya kawaida angekuwa
ni mtu mwenye kinyongo sana.
Hata hivyo Mandela alionesha huruma na
msamaha wa hali ya juu sana . Aliposhika
madaraka alihakikisha kuwa watu weupe
wanajihisi salama na kuondoa kabisa roho ya
kulipiza kisasi hasa kwa watu weusi ambao
waliumia sana mikononi mwa weupe kwa
karibu miaka 400. Anapoitwa “Baba wa
Taifa ” la Afrika ya Kusini haitwi hivyo kirahisi.
Mchango wake wa pekee kwa nchi yake
unamuweka katika nafasi ya pekee
kukumbukwa na vizazi vingi vijavyo . Hali hii
ya msamaha iligusa hata maisha yake
binafsi. Pamoja na kupata habari za mkewe
Winnie Mandela kukosa uaminifu Mandela
bado alihakikishia kuwa anapatiwa uwakilishi
wa kutosha kujitetea kwenye kesi iliyomkabili
ya utekaji na mauaji . Hata baada ya
kuachana naye Mandela na mkewe mpya
Graca Machel – aliyekuwa mke wa
marehemu Samora Machel ( Rais wa
Msumbiji aliyeuawa kwa njama za makaburu )
– Mandelea amekuwa na mahusiano mazuri
na ya utulivu na Winnie ambaye ameshiriki
vilivyo katika kumuuguza Madiba .
Dunia kwa hakika imepoteza shujaa wa haki
za binadamu, nyota ya Afrika na mfano wa
viongozi ambao waliweka maslahi ya watu
wao mbele zaidi kuliko furaha zao binafsi na
za familia zao. Wananchi wa Afrika ya Kusini
wanapomlilia wanaungana na mamilioni zaidi
katika bara la Afrika na Dunia ambao
wanakumbuka nafasi ya Mandela katika
maisha yao.
Kwa Watanzania wengi hasa waliokua miaka
ya sabini na themanini harakati za kutaka
Mandela afunguliwe na kukomeshwa kwa
utawala wa kikaburu zilikuwa ni sehemu ya
maisha yao. Hawa pia wanamshukuru Mungu
kwa maisha ya Mandela na wanaungana
kutoa rambirambi na pole kwa familia ya
Mandela na kumwombea pumziko la amani
baada ya maisha ya uchovu na kazi ngumu .
Watanzania wanaungana na ndugu zao wa
Afrika ya Kusini katika maombolezo haya;
wao wenyewe wanakumbuka vile vile jinsi
walivyoondokewa na Baba wa Taifa Mwalimu
Nyerere na jinsi akili ya jumla ya Taifa
ilivyoguswa lakini pia kuonekana kwa
kubadilika kwa taifa kwa kutokuwepo
Mwalimu. Ni wazi kuwa hata Afrika ya Kusini
nayo itapita huku ambapo ile Dhamira ya
Taifa ( Consciousness of a Nation) yaani
Mandela atakuwa hayupo . Njia pekee ya
kuhakikisha kuwa Afrika ya Kusini inazidi
kujijenga katika maisha ya kisasa na kuinua
watu wake kuelekea maendeleo ni lazima
kukumbuka umoja na udugu ambao Mandela
alipigania.
MUNGU AILAZE ROHO YAKE MAHALA PEMA
PEPONI
Friday, December 6, 2013
RIPOTI MAALUM : BURIANI NELSON MANDELA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment