SERIKALI ya Uganda tayari imeshaanza kulipa
deni lake kwa Tanzania la dola za Marekani
milioni 9.6 kati ya dola za Marekani milioni
18.4 ikiwa ni fidia kwa Tanzania kwa mchango
wake katika kumuondoa Idd Amin Dada Uganda
mwaka 1978.
Hayo yalibainishwa bungeni jana na Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Shamsi
Vuai Nahodha, wakati akijibu swali la msingi la
Mbunge wa Mbinga, John Komba (CCM).
Katika swali lake Komba alitaka kujua kama
Tanzania ilishaanza kudai fidia kwa Serikali ya
Uganda kutokana na mchango wake wa
kuisaidia nchi hiyo kumuondoa Idd Amin na
kumfanya Rais wa sasa Yoweri Museveni
kutawala kwa amani nchini humo.
Akijibu swali hilo, Nahodha alikiri kuwa
Tanzania ilipigana vita na Uganda kuanzia
mwaka 1978 hadi mwaka 1979 kutokana na
uvamizi uliofanywa na Uganda chini ya utawala
wa Idd Amin aliyevamia na kukalia sehemu ya
ardhi ya Tanzania mkoani Kagera.
“Kwa kuwa vita hivyo vilitokana na uvamizi wa
Idd Amin, baada ya vita kumalizika Serikali ya
Tanzania iliitaka Uganda kulipa fidia. Serikali
hiyo nayo ilikubali kuilipa Tanzania fidia hiyo,”
alisema Nahodha.
Alisema kwa bahati mbaya Serikali ya Uganda
haikutekeleza makubaliano hayo yaliyofanyika
mwaka 1979 hivyo Serikali ya awamu ya tatu ya
Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mstaafuma
William Benjamin Mkapa ilifanya majadiliano
tena na Uganda.
Alisema kutokana na majadiliano hayo Serikali
ya Uganda ilitakiwa kulipa fidia dola za
Marekani milioni 18.4 na hadi sasa Serikali hiyo
imeshalipa dola za Marekani milioni 9.6 fedha
ambazo ziliwekwa katika Mfuko Mkuu wa
Serikali na nchi hiyo kubakiwa na deni la dola
za Marekani milioni 8.8.
Nahodha alisema majadiliano baina ya Tanzania
na Uganda yanaendelea ili sehemu ya fidia
iliyobaki iweze kulipwa chini ya Wizara ya
Fedha ambayo ndio inayofuatilia deni hilo.
Akijibu swali la nyongeza la Komba la kuitaka
Tanzania imkumbushe Museveni juu ya namna
Tanzania ilivyosaidia nchi yake hivyo aache
kuihujumu kwa kusaidiana na Rais wa Rwanda
Paul Kagame, Nahodha alisema siku zote
Tanzania haimsaidii mtu ili kupata shukurani. “
Tanzania ni nchi ya kipekee sana, imebahatika
kupata viongozi wenye sifa kubwa duniani kama
Nyerere (Mwalimu Julius), kiongozi huyu
aliwahi kusema Waafrika ni ndugu na Afrika
yetu sote, tuliwasaidia Uganda kwa utu
hatutegemei zaidi,” alisisitiza.
Alisema hata juzi baada ya kifo cha Rais wa
zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela,
Tanzania ilitoa tamko la kumuenzi kwa
kusisitiza uvumilivu, jambo ambalo limeipatia
sifa kubwa Tanzania. “Naomba tuendelee
kuitunza sifa hii na si vinginevyo.”
Credit->Habari leo
Thursday, December 12, 2013
UGANDA YAANZA KUILIPA TANZANIA MABILIONI IKIWA NI FIDIA KWA MCHANGO WAKE KATIKA KUMUONDOA "IDD AMIN DADA" MWAKA 1978
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Sawa tanzania wamepanga kutugawia mitaji au vipi
ReplyDeleteMmmh wakubwa lzm wanenepe mwaka huuuuuuuu
ReplyDeleteMihela
ReplyDelete