Sunday, December 8, 2013

WATATU WAKAMATWA KWA KUPANGA MECHI UINGEREZA

Watu watatu wanazuiliwa na polisi nchini
Uingereza baada ya aliyekuwa mchezaji wa
Portsmouth kumwambia mwandishi wa habari
kuwa alihusika katika kupanga mechi.
Sam Sodje alirekodiwa kwenye kanda ya video na
mwandishi wa habari mmoja wa jarida la Sun
akizungumzia alivyompiga mchezaji wa timu
hasimu usoni katika ligi ya daraja la kwanza, ili
apate kadi nyekundu na kisha baadaye alipwe
pauni 70,000.
Alisema pia alipangia mchezaji mwingine aweze
kulipwa pauni 30,000 kwa kupokea kadi ya
manjano katika mechi ya ligi.
Klabu ya Portsmouth imeelezea kushtushwa sana
na madai hayo.
Katika Kanda hiyo liyorekodiwa kisiri, bwana
Sodje raia wa Nigeria, pia alidai ana uwezo wa
kupanga mechi za ligi kuu na kuwa yuko tayari
kupanga mechi katika kombe la dunia mwaka
ujao.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, msemaji
wa klabu hiyo, alisema kuwa ikiwa madai haya ni
ya kweli, basi ijulikane kuwa ni ya kushtua na
kushangaza sana , jambo la kupanga mechi bila
shaka linaathiri pakubwa maadili ya mchezo wa
soka.
Sodje hachezei tena klabu ya Portsmouth lakini
itambidi ashirikiane na maafisa wakuu kwa
uchunguzi.
Sodje aliondolewa uwanjani katika dakika ya 50
wakati wa mchuano kati ya Portsmouth na
Oldham Athletic kwenye ligi ya daraja la kwanza
tarehe 23 Februari mwaka 2013.

No comments:

Post a Comment

.