MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
(Chadema), kwa mara nyingine ameingia
matatani baada ya kushindwa kesi iliyofunguliwa
na mfanyabiashara raia wa Afrika Kusini.
Katika kesi hiyo, Zitto alituhumiwa kutoa madai
kupitia tovuti yake
www.zittokabwe.wordpress.com kuwa
mlalamikaji, Moto Mabanga alitoa rushwa ya
mabilioni ya fedha kwa maofisa wa Serikali ya
Tanzania ili kufanikisha kampuni ya Ophir Energy
kupata vitalu vitatu vya gesi mkoani Mtwara kati
ya mwaka 2004/2005.
Katika kesi hiyo ya madai Namba 153 ya 2013
iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam,
mfanyabiashara huyo pamoja na mambo
mengine alidai kulipwa fidia ya Dola za Marekani
milioni 5 ambazo ni sawa na Sh bilioni 8 za
Tanzania.
Katika hukumu iliyotolewa na Hakimu Mkazi
Mwandamizi, Sundi Fimbo, Novemba 21 mwaka
huu bila Zitto kuwapo, Mahakama ilijiridhisha
kuwa maneno yaliyoandikwa kwenye tovuti
binafsi ya Zitto na kwenye mitandao ya jamii
yalimkashifu mlalamikaji na mlalamikiwa
ameshindwa kuyathibitisha.
Mahakama hiyo imemtaka Zitto kuomba radhi
kwenye tovuti yake na mitandao ya jamii
ambako aliandika kashfa dhidi ya
mfanyabiashara huyo.
Pia imemuamuru mlalamikiwa pamoja na
washirika wake kuacha kwa njia yoyote ile
kuendelea kuandika na kusambaza habari zenye
kumkashifu mlalamikaji.
Mwanasiasa huyo kijana ambaye katika siku za
karibu amekumbwa na misukosuko ya kisiasa,
pia ameamriwa kumlipa mlalamikaji jumla ya Sh
milioni 3 kutokana na madhara yaliyotokana na
kashfa husika.
Awali, mlalamikaji alitaka kulipwa Dola za
Marekani milioni 5, lakini akashindwa
kuithibitishia Mahakama ni jinsi gani alipata
hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na
kashfa hiyo. Pia Zitto ametakiwa kulipa gharama
zote za kesi hiyo.
Alipoulizwa jana kama anakubaliana na hukumu
hiyo au anakusudia kukata rufaa, Zitto alijibu
kwa ufupi; “Sijaona hukumu wala sijawahi kufika
mahakamani.”
Julai mwaka jana, Mabanga alifikisha
malalamiko mahakamani akidai Zitto ameandika
taarifa zenye kumkashifu kwa kumhusisha na
utoaji mkubwa wa rushwa.
Mbali na kujihusisha na biashara sehemu
mbalimbali duniani, Mabanga amekuwa
akitumika kama kiunganishi kati ya wawekezaji
wakubwa na Serikali mbalimbali ikiwamo Serikali
ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Katika madai yake, aliitaka Mahakama
kumuamuru Zitto kutoka uthibitisho dhidi ya
madai ya kuwapa rushwa maofisa wa Serikali
katika mchakato wa kupata vitalu vya gesi wa
kampuni ya Ophir Energy.
Pia aliiomba Mahakama kutamka kuwa maneno
yaliyoandikwa na Zitto ambaye pia ni Waziri
Kivuli wa Fedha kwenye tovuti yake na mitandao
ya jamii si ya kweli bali ni kashfa.
Wakati hali ikiwa hivyo, wiki mbili zilizopita
Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kilimvua nyadhifa zote Zitto Kabwe
ikiwamo ile ya Naibu Katibu Mkuu.
Katika mkutano wa Kamati Kuu ya Chadema
uliofanyika Dar es Salaam, Mwanasheria Mkuu
wa chama hicho Tundu Lissu, alisema Zitto na
wenzake wamebainika kukihujumu chama kwa
kuanzisha mpango unaoitwa Mkakati 2013
ukilenga kukisambaratisha chama hicho, ili
kuwaondoa madarakani Mwenyekiti na Katibu
Mkuu wake.
Wengine waliovuliwa nyadhifa zao ni pamoja Dk.
Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha,
ambapo walipewa siku 14 wajieleze kimaandishi
kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi za kinidhamu
ikiwamo kuvuliwa uanachama.
-Mtanzania
Thursday, December 5, 2013
ZITTO MATATANI BAADA YA KUSHINDWA KESI YAKE YA KUTOA KASHFA DHIDI YA MFANYABIASHARA RAIA WA AFRIKA KUSINI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment