Tuesday, February 18, 2014

JINA LA OKWI LARUDISHWA KATIKA KAMATI YA TFF

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) ,
limemlalamikia mwanafamilia wa soka
mmoja kwa Kamati ya Maadili kutokana na
udanganyifu alioufanya katika suala la
usajili wa kiungo mshambuliaji wa Yanga,
Emmanuel Okwi .
Tayari TFF imepata ufafanuzi kutoka Fifa
kwamba Okwi anaweza kuendelea kuichezea
Yanga, lakini TFF imeibuka tena na kudai
Sabri Mtulla alilidanganya shirikisho hilo
kuhusu usajili wa Mganda huyo .
Akizungumza na Championi Jumatano , Ofisa
Habari wa TFF, Boniface Wambura , alisema
Mtulla analalamikiwa na TFF kwa madai ya
kuidanganya Kamati ya Sheria , Maadili na
Hadhi za Wachezaji kuwa hakukuwa na
pingamizi lolote juu ya usajili wa Okwi huku
akijua wazi kuwa jambo hilo si kweli .
“Kwa mujibu wa kanuni, malalamiko hayo
yamefikishwa kwenye Kamati ya Maadili
ambayo itachunguza ili kujiridhisha kama
yana msingi au la . Ikibaini kuna kesi ndipo
mlalamikiwa atafika mbele ya kamati hiyo , ”
alisema Wambura .
Hii ina maana kuwa jina la Okwi ambaye
amekuwa akijadiliwa mara kwa mara
limerudishwa tena kwenye kamati
kujadiliwa , ingawa maamuzi yoyote
hayataweza kumzuia kucheza .
Okwi anatarajiwa kuichezea Yanga mchezo
wa kwanza wa ligi kuu Jumamosi ijayo dhidi
ya Ruvu Shooting baada ya Fifa kuiruhusu
TFF kumtumia.
Okwi alisajiliwa Etoile du Sahel ya Tunisia
kutoka Simba kwa kitita cha dola 300 , 000
(zaidi ya milioni 480 ) fedha ambazo Simba
hawajazipata lakini baada ya muda mfupi
aliondoka klabu hapo na kujiunga na Villa
ya Uganda , ambayo ilimuuza kwenda Yanga
na utata mkubwa ukazuka.
Wambura pia alisema wanafamilia wengine
wanne wa soka ambao ni Riziki Majala ,
Army Sentimea, Oden Mbaga na Samwel
Mpenzu nao wanalalamikiwa kughushi
nyaraka ili kuhalalisha mtihani wao wa
utimamu wa mwili wa waamuzi .

No comments:

Post a Comment

.