Kuku wawili, mweusi kuzima nyota ya
mpinzani , nyeupe kujing'arisha .
Saleh Ally na Sweetbert Lukonge
SUALA la ushirikina katika soka limekuwa
likizungumzwa kama hadithi za kufikirika ,
wako ambao wanasema mambo hayo
hayatokei , lakini wako ambao wamekuwa
wakithibitisha kuwa hali hiyo inatokea .
Mganga
akiendelea kuandika majina ya Viongozi.
Suala la ushirikina linakuwa katika sehemu
mbalimbali, mfano wachezaji kwenda kwa
waganga wa kienyeji maarufu kama
wataalamu na kufanya kitu fulani ili
kuwadhoofisha wenzao au wachezaji
wanaocheza nao katika kikosi kimoja.
Wako ambao wamekuwa wakifanya kila
linalowezekana kuhakikisha wachezaji
wenzao wanaumia , katika soka suala hilo ni
maarufu kama ‘ misumari’ wakiwa na maana
kuwa anayeumizwa , basi anakuwa amepigwa
misumari.
Uchunguzi wa Championi kwa takribani
mwezi mmoja na ushee , limekuwa
likizunguka sehemu mbalimbali kufanya
uchunguzi, ishu kubwa ilikuwa ni
kuzungumza na watu mbalimbali na kutaka
kujua kuhusiana na suala la ushirikina .
Inaonekana pamoja na kuwa na mambo
mengi, suala hilo limegawanyika kwenye
mambo mengi lakini matatu ndiyo
yanaonekana kuchukua nafasi . Kwanza ni
kuroga ili kuhakikisha timu inashinda , lengo
hapa ni kuidhoofisha timu moja ili nyingine
ishinde .
Suala la pili ni mchezaji kuhakikisha mmoja
anaumia na kushindwa kabisa kufanya
vizuri ili kumpa nafasi yeye aendelee
kufanya vizuri na la tatu , mchezaji ni
kusafisha nyota yake na kuidhoofisha ya
mwenzake na hapo yeye atang ’ara na
kufanikiwa huku yule mwingine akifeli .
Katika watu mbalimbali ambao walifanya
mahojiano na Championi Ijumaa , wengi
wakiwa kutoka katika klabu kubwa za
Simba , Yanga , Azam FC , Mtibwa Sugar,
Coastal Union , wamekiri kuwa kweli
ushirikina hufanyika .
“Hauwezi kusema uache kufanya ushirikina,
sisi tumekuwa tukifanya kwa lengo la
kujilinda na kupambana na timu pinzani .
Kama wenzetu wanafanya hivyo , sisi
tukikaa kimya maana yake tunakubali
kuumia, ” anasema mdau mmoja kutoka
moja ya klabu kubwa za Tanzania.
“Uongozi unatutambua, kumekuwa hadi na
fungu letu na lengo ni zuri tu, kuilinda
timu yetu na kuisaidia kufanya vziuri,
kamwe hatulengi kumuumiza mtu, ”
anasisitiza.
Rekodi ziko nyingi sana kuhusiana na
masuala ya ushirikina , hadi wachezaji
Waafrika wale maarufu wanaocheza Ulaya
kama Didier Drogba, Samuel Eto ’ o na
wengine wamekuwa wakihusishwa na kufanya
hivyo.
Mwaka 2009, mwandishi wa makala haya ,
alishuhudia baadhi ya waganga wa kienyeji
nchini Ivory Coast wakiishi maisha ya juu
kutokana na mamilioni ya fedha
wanayoingiza. Uchunguzi wake ulionyesha
kuwa wana fedha nyingi kwa kuwa
wamekuwa wakifanya kazi ya kusafisha
nyota za wachezaji maarufu wa nchini hiyo
wanaocheza Ulaya kama Yaya & Kolo Toure ,
Drogba, Didier Zokora, Aruna Dindane na
wengine.
Hapa vipi kuhusiana na suala hilo,
Championi likaanza kukata mbuga likisaka
mganga wa kienyeji ambaye amewahi
kuifanya kazi yake hiyo vizuri kwa lengo la
kuwasaidia wachezaji kuosha nyota zao.
Uchunguzi ulionyesha mganga huyo kijana
na maarufu anapatikana eneo moja la
vitongoji vya Jiji la Dar es Salaam na kazi
ya kutafuta namba yake ikafanyika kupitia
ndugu yake. Baada ya makubaliano , siku ya
kwenda ‘ kumtibu’ mchezaji huyo ikapangwa .
Waandishi wawili wa makala haya , Saleh
Ally akajitambulisha kama meneja
anayeishi barani Ulaya na mchezaji ,
Sweetbert Lukonge ndiye mchezaji
anayetaka kwenda kucheza Ulaya, alitaka
nyota yake ing ’ are kuanzia hapa nchini,
baadaye Ulaya .
Miadi ikatengwa na siku ilipowadia , Meneja
(Saleh) ambaye lafudhi yake kidogo ina
Kiswahili cha shida kutokana na kuishi
Ulaya siku nyingi pamoja na mchezaji
(Lukonge ) walifika kwenye kitongoji hicho
na kupokelewa. Moja kwa moja ,
wakafikishwa hadi nyumbani.
Gari walilazimika kulipaki barabarani,
halafu wakaingia mitaa ya ndani ( si mbali
sana) ambako gari halifiki na kwenda
nyumbani kwa mganga huyo kijana , mahiri
‘kuwaponya ’ wachezaji ili waweze kufanya
vizuri katika soka .
Baada ya kufika , mganga aliuliza shida
yao, maelezo ya meneja yalilenga
kumsaidia mchezaji huyo ili amfunike
mchezaji mwingine ambaye alikuwa
akimzuia kupata namba kwa kuwa huyo
meneja anataka mchezaji wake ang ’ are .
Mganga aliwahakikishia kuwa kila kitu safi
kabisa na ndani ya siku chache baada ya
tiba ya siku hiyo . Mambo yangekuwa mazuri
lakini kulikuwa na bidhaa za kununua siku
hiyo ili kuanza tiba .
Vifaa vilivyotakiwa ni kuku wawili, weupe na
weusi , kitambaa , kipande cha sanda
ambacho kimefukuliwa baada ya mtu
kuzikwa. Yai na vingine ambavyo tayari
viliandaliwa na mganga huyo .
Ikatolewa Sh 20 , 000 kwa ajili ya kununuliwa
kuku wawili na bei ya ‘ matibabu ’ hayo
ilikuwa ni Sh 300, 000 hadi 400, 000 ingawa
kulikuwa na makubaliano kwa vile mganga
anaonyesha si mtu wa tamaa na anayetaka
‘kusaidia ’ watu.
Makubaliano yanafikiwa , meneja na
mchezaji wake wanalazimika kumsubiri
mganga anayefunga safari kwenda
kununua kuku , baada ya kurejea anaomba
muda mchache kuandaa vifaa vyake kabla
ya kuanza kazi .
Baada ya hapo , mtoto mdogo anatumwa
kuwaita wahusika (meneja , mchezaji)
ambao baada ya kuingia kwenye chumba
ambacho hufanyika kazi za mganga
wanaelezwa kazi itakavyofanyika chumbani
humo na baada ya hapo ni safari ya
kwenda makaburini ili kuimaliza kazi hiyo
huko.
Kidogo wawili wanaingiwa hofu , lakini
mganga anawasisitiza hawapaswi kuwa
waoga hata kidogo kwa kuwa kila kitu
kitakwenda vizuri huku akiwatolea mfano
wachezaji maarufu wa Yanga, Simba na
timu nyingine ambao wamewahi kufika na
kupata tiba hiyo ya kuosha nyota .
“Hata watu wa kawaida na maofisa
wanafika hapa kwa ajili ya kupata huduma
hii , ondoeni hofu na mambo yatakwenda
vziuri, ” anasema mganga huyo kijana .
Suala la makubaliano ya bei linafanyika na
anakubali kupunguza bei ingawa wahusika
ni watu wanaoishi ‘Ulaya ’. Na kwa nafasi
hiyo , meneja anaomba kupiga picha za
kumbukumbu ambazo ataenda nazo Ulaya
kwa kuwa kule ni mambo tofauti na huenda
itamsaidia ‘ fundi’ kupata wateja zaidi
kutoka ughaibuni . Anapewa ruhusa.
Kazi inaanza , mchezaji anakalishwa kwenye
kigoda ( lazima akae kwenye kiti juu , ili
nyota yake ipande) , anafunikwa shuka
lenye rangi nyeupe) . Kazi inaanza .
Mganga huyo au fundi anachukua vitu
kama ukindu anavifunga na kufunga
kwenye miguu ya mchezaji ambaye amevaa
jezi ya Liverpool , butka nyeupe na viatu
Adidas rangi ya njano . Anachukuliwa kuku
mweupe na mweusi anaachwa pale chini .
Yule kuku mweupe, huku ubani umefukizwa
kwenye chetezo kikubwa kama bakuli, moshi
unaanza kufuka . Mchezaji anamchukua
kuku huyo na kumuweke kwenye moshi
unaofuka, ghafla kuku analala kama mlevi
aliyezidiwa kinywaji na anafanya hivyo
huku akitakiwa kunuwia anataka apate
nini, anafanya hivyo.
Wakati huo, mganga anaendelea kuandika
majina ya viongozi wa timu ya mchezaji
huyo ambao wanatakiwa kumsahau yule
mchezaji mwingine na kumfikiria mchezaji
aliyeletwa na meneja .
Baada ya hapo , karatasi lenye majina
anakabidhiwa mchezaji huyo mkononi .
Halafu analiweka juu ya moshi unaofuka
kupitia chetezo, na mganga anachukua
dawa aina mbili pamoja na mafuta fulani
hiyo , anamwaga juu ya karatasi na ghafla
moto unalipuka .
Meneja jasho linamtoka na mchezaji
halikadhalika anaonyesha kuwa na hofu
kuu. Lakini mganga anaendelea na kazi
yake kwa ustadi mkubwa huku akisisitiza
wakati huo ndiyo mwanzo kabisa kazi
inaanza kwani kuna mengi kama kumlisha
kitu kuku na kumchinja , pia kwenda
makaburini kuchimbia vitu kwenye
makaburi .
HALI hiyo inatisha, hiyo ni sehemu kati ya
mambo ambayo hufanyika kwenye mchezo
wa soka na wahusika wanasisitiza si kwa
ajili ya kumdhuru mtu badala yake ni
kusaidia au kumlinda mtu. Usikosea
CHAMPIONI JUMATATU kujua mwendelezo wa
mambo yatakavyokuwa kwa mchezaji huyo
na meneja pia .
Friday, February 21, 2014
RIPOTI MAALUM : WAGANGA WA KIENYEJI WANAVYOFANYA KAZI NA WACHEZAJI YANGA , SIMBA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment