Tuesday, March 4, 2014

MASKINI JACK HALI MBAYA

MODO mwenye mvuto Bongo Jacqueline
Patrick ‘ Jack ’, ambaye yuko mahabusu ya
Gereza la Qincheng nchini China kwa madai
ya kunaswa na madawa ya kulevya nchini
humo, anazidi kuteseka , safari hii akidaiwa
kukabiliwa na tatizo kubwa la kiafya .
Jacqueline Patrick ‘Jack ’ .
Kwa mujibu wa chanzo chetu , Jack
anasumbuliwa na ugonjwa wa kukosa hamu
ya kula, hali iliyomfanya apoteze uzito wa
kilo kumi huku akikabiliwa na tatizo lingine
la kupungua kwa kasi ya mapigo ya moyo .
KAMA HALI ITAENDELEA
Chanzo kimesema kuwa endapo hali ya
kuzorota kwa afya hiyo kutaendelea, Jack
anaweza kujikuta katika tatizo kubwa zaidi
ambalo linaweza kusumbua kwenye
mwenendo mzima wa kesi yake.
“Kusema kweli kuhusu maisha ya mahabusu
si mabaya sana kwake, hateswi kwa kupigwa
wala hanyimwi chakula, ila hana uhuru
binafsi, ni kama amefichwa , naamini
matatizo hayo ya kiafya yanatokana na
uzito wa kesi yake , ” kilisema chanzo hicho .
MLOLONGO WA MAMBO
Habari zaidi zinadai kwamba kesi ya msingi
ya staa huyo kudaiwa kukutwa na madawa
ya kulevya itaanza kusikilizwa rasmi
Septemba, mwaka huu baada ya
mwanasheria wake kukamilisha taratibu
zote.
“Ile kesi yake sasa ni Septemba mwaka huu .
Si unajua hajawahi kupandishwa kizimbani
kuulizwa kama ni kweli alikamatwa na unga
au la !” kilisema chanzo hicho .
Jack Patrick akiwa amefunikwa uso baada
ya kukutwa na pipi za heroin tumboni nchini
China.
WAKILI WAKE ANATOKA HONG KONG
Taarifa zaidi zinasema kuwa wakili wa
mrembo huyo anatoka jijini Hong Kong
nchini humo ambako ndiko kwenye
wanasheria wazuri kwa kiwango cha kesi
yake ya unga .
KUMWONA NI KWA AHADI
Ikazidi kudaiwa kwamba kuna Mtanzania
mmoja tu ambaye amekuwa na fursa ya
kumuona modo huyo na kabla ya kwenda
lazima aombe na kupewa ‘apointimenti ’
maalum.
WALIOMTUMA WAMPIGA CHENGA , WALA
‘BATA’
Tofauti na kwa Video Queen wa Bongo,
Agnes Gerald ‘Masogange’ ambaye naye
aliwahi kupata msala mkubwa kama huo
nchini Afrika Kusini , Julai , mwaka jana
ambapo ‘mabosi ’ wake walikuwa mstari wa
mbele kumhangaikia , Jack anasota
mwenyewe.
Habari zinasema kuwa hakuna cheni yoyote
kutoka kwa watu ambao wanatafsiriwa kuwa
ni waliomtuma kwani wanaosumbuka ni watu
wake wa karibu, wakiwemo ndugu zake .
Juzi , Risasi Mchanganyiko lilizungumza na
mtu wa karibu sana na mtuhumiwa huyo
ambapo alikiri Jack kuwa na hali ngumu
katika kesi yake hiyo huku akisema kwamba
watu wanaodaiwa ndiyo mabosi wake
wanakula ‘bata ’ tu jijini Dar es Salaam .
“Unajua tatizo la biashara ya unga ni hapo
tu! Wewe unayebeba ukinaswa ni juu yako,
waliokutuma wao wanachofanya ni
kuthibitisha tu kuwa ni kweli umekamatwa
maana wapo wanaodaiwa wamekamatwa
kumbe si kweli , wanaingia mitini na mzigo , ”
alisema mtu huyo .
SABABU ZA MOYO KUSHINDWA KUSUKUMA
DAMU
Juzi , gazeti hili lilimtafuta daktari mmoja
wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ( jina lipo )
na kumuuliza tatizo la moyo kushindwa
kusukuma damu ambapo alisema:
“Moyo kushindwa kusukuma damu kwa
mwendo wa kawaida husababishwa na
shinikizo la damu lisilodhibitiwa, mgonjwa
kushindwa kudumisha udhibiti wa maji
mwilini, chakula au dawa.
“Sababu nyingine ni upungufu wa damu na
utoaji wa kiwango cha juu cha homoni za
koromeo ambazo zinaleta maumivu ya ziada
kwenye misuli ya moyo , utumiaji mwingi wa
vimiminika au ulaji wa chumvi uliopitiliza
na utumiaji wa dawa ambazo husababisha
uwekaji wa maji mwilini kama vile
Hiazolidinedione.”
KUHUSU KUKOSA HAMU YA KULA
Kwa mujibu wa daktari huyo , tatizo hilo
humkumba mtu anapokuwa katika msongo
mkubwa wa mawazo kutokana na jambo zito
linalomkabili , ambalo halina mlango wa
kutokea.
TUKUMBUKE
Mrembo huyo alikamatwa Desemba 19 ,
mwaka jana katika Uwanja wa Ndege wa
Macau, China akitokea Bangkok , Thailand
akiwa na kete 57 ( kilo 1 . 1 ) za heroin
tumboni zikiwa na thamani ya jumla ya
zaidi ya shilingi milioni 300.
Awali ilidaiwa kuwa kesi yake ingeanza
kusikilizwa mwaka 2016 baada ya yeye
kujifunza Kireno ( lugha inayotumika
Macau) kwa miaka miwili .

No comments:

Post a Comment

.