CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua
kuwatosa mawaziri saba wanaotajwa kuwa ni
mizigo kwa serikali inayoongozwa na chama
hicho.
Hatua hiyo ya kuwatosa mawaziri hao
waliohojiwa na Kamati Kuu (CC), iliyokutana juzi
mkoani Dodoma, inalenga kukinusuru chama
katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika
mwaka 2015. Mawaziri waliowekwa kwenye
kikaango cha kung’olewa ni Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Christopher Chiza; Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru
Kawambwa; Waziri wa Utumishi, Celina Kombani
na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Wengine ni Waziri wa Viwanda na Biashara,
Abdallah Kigoda; Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mathayo David Mathayo na Naibu Waziri wa
Fedha, Saada Mkuya.
Tanzania Daima Jumapili, imedokezwa kuwa
baadhi ya viongozi wa chama hicho wamekuwa
wakitaka mawaziri wanaofanya vibaya kwenye
wizara zao wawajibishwe kila mara ili kuiepusha
serikali kuchukiwa na wananchi.
Inadaiwa wanataka utaratibu uliokuwa ukifanywa
miaka ya nyuma na chama chini ya utawala wa
Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere
wa kuwaita mawaziri na kuwahoji kwenye vikao
vya chama urejewe.
Hoja kubwa wanayoijenga ni kuwa chama ndicho
kinachopata wakati mgumu katika chaguzi kwa
sababu ya watendaji au mawaziri kutowajibika
ipasavyo.
Inaelezwa kwa muda mrefu kumekuwa na
mipango ya kuwaondoa mawaziri hao, lakini
mazingira ya kuwaondoa ndiyo yamekuwa
yakikosekana. Lakini hivi sasa mkakati
umeshaiva. Inadaiwa ziara za kuimarisha chama
zilizofanywa na viongozi wa CCM katika mikoa
ya Ruvuma, Mbeya, Njombe na Mtwara ndizo
zimetumika kuandaa mashtaka ya mawaziri hao
ambayo waliyajibu walipoitwa kujitetea.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa
licha ya utetezi huo, Kamati Kuu imemtaka Rais
Jakaya Kikwete apime hoja zilizotolewa na
wajumbe wa CC kama mawaziri hao wanafaa
kuendelea na nyadhifa zao.
Uamuzi wa CC
Kikao cha CC kilichoketi juzi, kimemtupia mzigo
wa kuwang’oa mawaziri Rais Kikwete ambaye
ndiye aliyewateua.
Akizungumza na waandishi wa habari, jana jijini
Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi,
Nape Nnauye, alisema CC imetoa mapendekezo
kwa Rais Kikwete ambaye ndiye mwenye hatima
ya mawaziri hao.
Alisema Rais Kikwete ni mamlaka ya uteuzi wa
mawaziri na ndiye atakayeamua kuwaadabisha,
kuwasukuma au kuwaondoa madarakani
mawaziri mizigo.
“Aliyewaweka ndiye atakayewaondoa, Kamati
Kuu haijamwabia awaondoe, inachokifanya ni
kushauri tu. Lakini madaraka yote anayo rais
aliyewachagua.
“Kwa mfano Waziri wa Chakula, Kilimo na
Ushirika hajafika kwa muda wa miaka minne na
nusu mkoani Ruvuma ambako ndiko kuna ghala
la chakula…, tulipofika Tunduma tulikuta foleni
pale mizani eti watumishi wanafanya kazi kwa
saa 9, lakini sasa wamebadilisha utaratibu huo
wanafanya kwa saa 24 baada ya sisi kwenda,”
alisema.
Nape akiwa katika ziara ya siku 26 mikoa
mbalimbali, aliwataja mawaziri hao ambao
wamekuwa mizigo katika serikali ya Rais
Kikwete na kumtaka awatimue.
Hata hivyo Waziri Chiza na Kawambwa walisema
kuwa hawafanyi kazi kupitia majukwaa ya siasa
na wanasubiri kuitwa na Kamati Kuu, ili waieleze
wanavyofanya kazi.
Waziri Kawambwa, alijinasibu kwa kujifafanisha
na mti wenye matunda ambao hauishi kupigwa
mawe kila kukicha. Waziri Chiza alimtaka Nape
aache kukimbilia kuzungumza hadharani juu ya
madai ya wakulima wa korosho na badala yake
atafute sababu ya wakulima hao kutolipwa na
serikali. Mabadiliko ya mawaziri Kama Rais
Kikwete ataamua kulifanyia mabadiliko Baraza la
Mawaziri itakuwa ni mara ya tatu, ambapo
mwaka 2008, alilivunja kutokana na aliyekuwa
Waziri Mkuu Edward Lowassa kujiuzulu kuguswa
na kashfa ya kuipa zabuni ya kuzalisha umeme
wa dharura Kampuni ya Richmond.
Mabadiliko mengine aliyafanya Mei mwaka jana
baada ya wabunge na wadau mbalimbali
kushinikiza kuondolewa kwa mawaziri
waliodaiwa kutowajibika ipasavyo.
Maagizo mengine ya CC
Kamati Kuu pia imeiagiza serikali iangalie upya
upatikanaji wa pembejeo za ruzuku kwa
wakulima wa pamba nchini. “Chama kimeiagiza
serikali kutowalazimisha wakulima kutumia
mbegu ya Quiton badala yake elimu itumike zaidi
badala ya nguvu,” alisema Nape.
Aliongeza kuwa CC imeitaka serikali kuangalia
upya urasimu katika uwekezaji wa viwanda
nchini hasa vinavyoongeza thamani ya mazao na
kutoa ajira nchini.
Nape aliongeza kuwa kuhusu kilimo cha mkataba
kwa wakulima wa pamba, serikali imetakiwa
kuratibu utaratibu wake ikiwemo
kutowalazimisha.
Kuhusu wakulima wa korosho, alisema kuwa
kamati hiyo imeisisitiza serikali kujipanga
kutatua tatizo la korosho na kuhakikisha
inabanguliwa nchini.
“Serikali inatakiwa kuangalia upya orodha ndefu
ya makato kwa wakulima, hasa wa korosho na
vyama vya msingi au mamlaka zinginezo ili
kuondoa makato yasiyo ya lazima na kuongeza
kipato cha mkulima.
“Kuhusu pembejeo za ruzuku Kamati Kuu
imepokea taarifa ya malalamiko ya wakulima juu
ya ufanyaji kazi wa mbolea ya Minjingu na
kuagiza wananchi wawe huru kutumia mbolea
wanayoitaka badala ya kulazimishwa,” alisema.
Kwa upande wa wakulima wa mahindi, Nape
alisema kuwa serikali imetakiwa kumalizia
malipo yaliyobaki na kuhakikisha wanakomesha
utaratibu wa kuwakopa wananchi mazao yao
bila kuwalipa.
“Utaratibu uwekwe wa kufanya tathimini
mapema ya mahitaji na uwezo wa kununua
mahindi wa serikali ili kuepusha utaratibu wa
kuchukua mahindi ya wakulima bila kuwalipa,”
alisema.
Nape alisema kwa upande wa madai ya walimu,
CC imeiagiza serikali kukamilisha uhakiki wa
madai hayo na kuwalipa haki zao ikiwemo
kuhakikisha madeni hayazaliwi tena.
Kamati hiyo pia imekemea watendaji wachache
wanaojihusisha na ubadhirifu kwenye
halmashauri mbalimbali nchini.
“Serikali imeshauriwa kuangalia upya sheria
kama zinakidhi mahitaji ya wakati na mazingira
ya sasa ili kuongeza uwezo wa udhibiti na
kuokoa pesa za walipakodi zinazopotea kwa
walafi wachache kwenye halmashauri mbalimbali
nchini,” alisema Nape.
Source: Tanzania Daima
Sunday, December 15, 2013
CCM KIMENUKA, MAWAZIRI SABA WANAOSEMEKANA KUWA MZIGO HATARINI KUNG'OLEWA, MAJINA YAO HAYA HAPA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment