Tuesday, December 10, 2013

MAKALI YA KILIMANJARO STARS YAIPA TEAM YA KENYA MCHECHETO-LAZIMA WAKAE


KENYA imeingia mchecheto na makali ya
Kilimanjaro Stars na sasa imebainika kwamba
Kocha Adel Amrouche ndiye aliyesisitiza mechi
ikachezwe Machakos badala ya Mombasa.
Kenya itacheza na Stars kesho Jumanne kwenye
mechi ya nusu fainali ya Chalenji kwenye Uwanja
wa Kenyatta mjini Machakos.
Awali nusu fainali hiyo ilikuwa ichezwe hapa
Mombasa, lakini kutokana na hali ya joto
ambayo inaibeba Tanzania na kukaa vibaya kwa
wachezaji wa Kenya wanaoishi Nairobi kwenye
baridi ndio maana mechi hiyo imeahirishwa.
Baada ya mechi dhidi ya Rwanda ambapo Kenya
ilishinda bao 1-0, Adel alikiri kwamba; “Hali ya
hewa ya Mombasa si nzuri kwetu ni joto kiasi na
wachezaji wangu hawajazoea.”
Habari za ndani zinadai baada ya Uwanja wa
Kisumu kushindikana kumalizika kwa wakati
waandaji walipanga mechi za nusu fainali
zichezwe Mombasa na fainali ikachezwe Nyayo
mjini Nairobi lakini kwa hali waliyoiona katika
mechi za juzi Jumamosi wenyeji wakaamua
kupeleka mechi ya Stars Machakos. Mechi
nyingine ya nusu fainali itachezwa mjini
Mombasa.
Habari za ndani zinadai kwamba Adel
amewaambia viongozi wake kwamba endapo
Kenya ikicheza na Stars mjini Mombasa itakuwa
kwenye wakati mgumu kutokana na Tanzania
kuzoea hali ya joto na vilevile ina sapoti kubwa
Mombasa kwavile ni jirani na Tanga.
Kenya iko kwenye presha ya kufuzu fainali kwani
siku ya fainali nchi hiyo itakuwa ikisherehekea
Jubilee ya miaka 50 ya uhuru wake.
Wakati huohuo, Zambia iliitoa Burundi kwa
penalti 4-3 katika mchezo wa robo fainali
uliofanyika jana Jumapili hivyo kutinga nusu
fainali.

No comments:

Post a Comment

.