Tuesday, December 10, 2013

NILIPELEKWA MUHIMBILI ILI NIINGIZWE MOCHWARI


INAWEZEKANA wapo wagonjwa
wanaopelekwa chumba cha kuhifadhia maiti
( mochwari ) wakiwa hai. Huenda wengine
hufia humo baada ya kuzidiwa na baridi la
chumba hicho sambamba na kukosa hewa .
Piga picha ni wewe !
Lakini kwa kijana Anina Shaban ( 28) mkazi
wa Kijiji cha Mbugu Wilaya ya Kilombero
mkoani Morogoro, yeye alibahatika , kwani
aliishia kwenye lango la kuingia mochwari
akidhaniwa ameshakufa .
Mkazi wa Kijiji cha Mbugu Wilaya ya
Kilombero mkoani Morogoro , Anina Shaban
( 28 ) akiwa wodini.
Akizungumza na mwandishi wetu hivi
karibuni akiwa ndani ya wadi ya Sewa Haji
kitengo cha MOI katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili , Dar alikolazwa kwa miezi 9 sasa ,
Anina anasema :
“Siwezi kuisahau siku ile , ninachoweza
kusema kwa urahisi sana ni Mungu tu ndiye
aliyependa nisife kwa wakati asiokubaliana
nao, vinginevyo leo ningekuwa kaburini .
“Ilikuwa mwezi wa tatu, tarehe ishirini na nne
nakumbuka , siku hiyo nilitua hapa Dar kwa
mara ya kwanza nikitokea kijijini kwetu .
“Lengo la kuja Dar lilikuwa kutafuta maisha
mazuri , maana vijana wenzangu
waliotangulia kuja kila waliporudi kusalimia
waliniambia maisha bora yapo kwenye Jiji la
Dar es Salaam.
Moja ya mguu uliovunjika.
“Niliamini kwani hata mavazi yao yalionesha
kwamba kweli wana maisha mazuri . Sasa ni
nani asiyetaka maisha mazuri ? Ndipo
nikaamua kuja Dar siku hiyo .
“Lakini ndoto zangu ziligonga mwamba mara
tu niliposhuka Kimara . Nilivuka barabara
kwenda upande wa pili nikiwa na begi langu
lenye nguo mbili tatu , ghafla daladala
lilitokea na kunigonga , nikaanguka na
kupoteza fahamu! Ilikuwa ajali kubwa sana .
“Nilipopata fahamu nilijikuta nikiwa hapa
Muhimbili , lakini nikiwa katika hali isiyokuwa
ya kwangu , mikono , miguu ilifungwafungwa .
Nilianza kulia huku nikiwa sijui hapa ni wapi .
“Daktari mmoja alipita na kuniona nikilia ,
akaja na kuniuliza kilichoniliza, nikamjibu hali
nilionayo, ndipo akanisimulia kwamba nilipata
ajali mbaya sana Kimara wakati nikivuka
barabara.
“Kilichonishangaza zaidi ni pale
nilipomuuliza ajali hiyo ilitokea lini ,
akaniambia mwezi mmoja uliopita . Ina
maana mimi nilikuwa katika hali ya
kutojitambua kwa muda wote huo.
Anina Shaban , ndani ya wodi ya Sewa Haji
kitengo cha MOI katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili, Dar .
“Cha ajabu , aliniambia nilifikishwa hapa si
kama majeruhi bali kama maiti ya mtu
aliyekufa kwa kugongwa na gari .
“Daktari huyo alisema walionileta kila mmoja
alijua nimeshaaga dunia kufuatia ajali ile .
Hivyo nilikuwa napelekwa moja kwa moja
mochwari .
“Daktari aliendelea kunieleza kuwa hakuna
aliyejua kwamba bado nilikuwa hai kwani
nilikuwa siangaliki kutokana na majeraha
makubwa niliyoyapata .
“Hata hivyo , kabla sijaingizwa mochwari
daktari mmoja alitaka kujiridhisha kwanza
kama kweli nilishafariki dunia , ndipo
akagundua kuwa bado nilikuwa hai kwani
nilikuwa napumua kwa mbali sana .
“Nilikuwa nimeumia vibaya mno . Nilivunjika
mikono yote, tena mara mbilimbili , nilivunjika
miguu yote na mbavu tatu .
“Nilifikishwa hospitalini nikiwa nimekunjwa
kama mtu anavyobeba nyama kwenye mfuko
wa rambo . Mwacheni Mungu aitwe Mungu
jamani, siamini kama kweli leo hii naweza
kukaa mwenyewe .
“Nilijiuliza nilipata wapi mkosi huo? Mbona
niliwaaga vizuri tu wazazi wangu kwamba
nakuja Dar kutafuta ajira na walinikubalia
kwa vile katika watoto watatu katika familia
yetu, mimi ndiyo mtoto wa kwanza na wote
tulikuwa nyumbani tukiendelea na kilimo cha
jembe la mkono .
“Nilijua hapa Dar ningepata kibarua hata cha
kuwakatia ng ’ ombe majani au kuwasombea
wajenzi matofali lakini kwa bahati mbaya
sikuyafikisha malengo niliyoyakusudia .
“Kinachoniuma na kunitoa machozi ni
kuwaona wagonjwa wenzangu
wanatembelewa na ndugu zao, wanawafariji
na kuwaletea vyakula lakini kwa upande
wangu hakuna hata mmoja .
“Kule kijijini wazazi hawana simu, mimi hapa
pia sina simu, ni vigumu kuwajulisha, nahisi
wanaamini tayari nimeshapata kibarua lakini
siwakumbuki.
“Wangejua wangenifuata kunichukua na
kunirudisha kijijini kwetu , ” Anina alisema na
kuanza kulia .
“Wagonjwa tuliolazwa nao wengi
wameshapona na kuruhusiwa kurejea
makwao. Lakini nasikitika kwamba nilitoka
nyumbani mzima nitarudi na ulemavu, ” akalia
tena .
“Nitakwenda kuwapa wazazi wangu kazi
ngumu ya kunitunza kama mtoto mdogo ,
hakuna jinsi inabidi niyakubali matokeo ,
najua huu ndiyo mwisho wangu wa utafutaji ,
nimebakia mtu wa kitandani , sikuyapenda
maisha haya bali ndivyo Mungu
alivyonipangia natembea lakini si kama
zamani, ” alisema kijana huyo.
Aliwaomba Watanzania ambao wangependa
kumsaidia watumie namba hii 0713 413098 .
Naye Afisa Mkuu Msaidizi Mambo ya Jamii
Kitengo cha Mifupa MOI , Matua Frank
alisema Anina anaendelea vizuri na wakati
wowote wanaweza kumsafirisha kwenda
kwenda kijijini kwao .
“Kwa sasa tunajiandaa kumsafirisha ,
tumempatia matibabu kwa kipindi chote
hicho kwa gharama ya hapa hospitali hadi
sasa amepata nafuu kwa kiasi fulani, ”
alisema Frank .

No comments:

Post a Comment

.