Monday, December 16, 2013

Okwi asaini Yanga SC


Na Khatimu Naheka
USAJILI wa kishindo , Yanga imefanya kufuru
kwa kufunga dirisha dogo la usajili kwa
kumsajili kiungo mshambuliaji wa zamani wa
Simba, Emmanuel Arnold Okwi na ataanza
kuichezea klabu hiyo kwenye mzunguko wa
pili wa Ligi Kuu Bara.
Okwi, ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa
ya Uganda , The Cranes , amesaini kuichezea
Yanga kwa miaka miwili na nusu na
Shirikisho la Soka la Uganda ( Fufa )
limemuidhinisha rasmi kuwa mchezaji wa
Jangwani.
Emmanuel Okwi akiweka alama ya dole
gumba mbele ya Mjumbe wa Kamati ya
Mashindano wa Yanga , Musa Katabaro
( kushoto) wakati akisaini mkataba wa
kuichezea Yanga miaka miwili na nusu
mpaka mwishoni mwa msimu wa 2015/2016 .
Kulia ni Mwanasheria /Meneja wa Okwi ,
Edgar Agaba .
Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga,
Abdallah Bin Kleb, amelithibitisha hilo kwa
Championi Jumatatu na taarifa zinasema
Okwi atatua nchini keshokutwa .
“Kweli tumemsainisha Okwi kwa muda huo
na kila kitu kiko safi, tumefuata taratibu zote
kupitia mtandao wa Fifa wa uhamisho na
tumepata ITC , hivyo Okwi ni mchezaji halali
wa Yanga, ” alisema Bin Kleb .
Taarifa zinaeleza Yanga imemwaga zaidi ya
Sh milioni 180 ili kumpata Okwi ambaye
anajulikana kwa kasi, krosi safi na uwezo wa
kufunga mabao katika wakati mgumu.
Awali, Simba ‘ ilimuuza’ Etoile du Sahel ( ESS )
kwa kitita cha dola 300, 000 ( Sh milioni 480 )
lakini malipo yamekuwa hadithi na uongozi
umekuwa mkali sana kuhusiana na hilo.
Baadaye akasusa kuichezea ESS kutokana na
kutolipwa mshahara wake , baadaye akarejea
SC Villa ya kwao Uganda ambako Shirikisho
la Soka la Kimataifa ( Fifa ) likamuidhinisha
acheze kwa mkopo.
Taarifa nyingine zinasema Okwi alisaini rasmi
kuichezea Yanga Jumatano iliyopita na kila
kitu kilifanyika jijini Kampala baada ya ‘ jeshi ’
la usajili la Yanga kuvamia mjini humo na
kumaliza zoezi hilo.
Kila kitu kikafanywa siri kubwa kwa kuwa
Yanga ilitaka kupata uhakika kwa kupokea
ITC ambayo imepatikana jana ikiwa ni siku
ya mwisho ya dirisha dogo la usajili .
Okwi alikuwa ‘ roho’ ya ushambuliaji Simba,
kipenzi cha mashabiki Msimbazi na tishio
kwa Jangwani, lakini sasa huenda mambo
hayo yakageukia upande wa pili .

No comments:

Post a Comment

.