Sunday, December 8, 2013

YULE MTOTO ALIYETESEKA AFARIKI DUNIA GHAFLA


Mtoto Suleiman Rajab enzi za uhai wake.
Na Imelda Mtema
MASKINI ! Yule mtoto Suleiman Rajab
aliyeteseka muda mrefu akisumbuliwa na
uvimbe mkubwa mguuni huku mamia ya
Watanzania wakijitolea kuchanga fedha kwa
ajili ya matibabu nchini India amefariki dunia
ghafla nyumbani kwao Ukonga- Kivule , Dar .
Akizungumza kwa masikitiko makubwa baada
ya kifo hicho, baba mzazi wa marehemu,
Rajab Upinde alisema kwamba mtoto wake
huyo hakuwa anasumbuliwa na kitu chochote
zaidi ya uvimbe uliokuwa mguuni lakini
alishikwa na ugonjwa wa ghafla na kufariki
dunia.
Baba huyo alisema kwamba Kampuni ya
Global Publishers kwa kushirikiana na Hoyce
Temu kupitia kipindi chake cha Mimi na
Tanzania kwenye Runinga ya Chanel Ten
walifanya jitihada kubwa za kukusanya
michango ambayo ilifanikisha maandalizi ya
safari ya matibabu India .
“Naumia sana kwa vile kila kitu kilikuwa
tayari. Tulikuwa tunasubiri siku ya kuondoka
tu . Global Publishers na Hoyce wamefanya
kazi kubwa kukamilisha safari ya India lakini
ndiyo hivyo Mungu kampenda zaidi kiumbe
wake, ” alisema baba huyo kwa uchungu .
Akizungumzia kifo cha mtoto wake , baba
huyo alisema kuwa siku ya tukio Sele
aliamka akilalamika kichwa kinamuuma
ambapo walimpa dawa za kutuliza maumivu .
Alisema aliporejea kutoka kazini mkewe
alimwambia kuwa Sele alikuwa akilalama
kuwa miguu inawaka moto ambapo alimfuata
mwanaye chumbani ambaye aliomba aitiwe
shehe.
Shehe alipofika alimuombea na baada ya
muda aliwaita wadogo zake na kuwaambia
yeye anakufa kwani anajisikia vibaya mno .
Baba huyo aliendelea kusema kuwa akiwa
amekaa nje alisikia mwanaye mwingine
akimuita aingie ndani kwani hali ya Sele
ilikuwa imebadilika na alipoingia alimkuta
mwili wote umelegea ambapo aliita majirani
ili wamsaidie , walipoingia ndani walimkuta
ameshafariki dunia .
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali
pema peponi. Amina.
“ Ki ukweli sikuweza kuamini macho yangu
kama mwanangu ndio ameniaga kwani
nilikuwa na ndoto nyingi za kumuona akipona
tena na kuwa mzima kama walivyo watoto
wengine” alisema baba huyo.
Kampuni ya Global Publishers kwa
kushirikiana na kipindi cha Mimi na Tanzania
kinachorushwa kupitia Televisheni ya Channel
Ten na mwanadada Hoyce Temu , na kwa
watanzania wote walio nje ya nchi kwa
kujitahidi kutoa michango yao Mungu
awabariki sana .

1 comment:

  1. Kila kitu nimpango wa Mungu akipanga jambo linatokea kabla hawajapoteza pesa akamchukua maana kifo kipo na kila nasi itaonja na kila mtu anaondoka kwa numna yake hata angepelekwa kama ilipangwa kufa angekufa so wamshukuru Mungu kwa kila jambo

    ReplyDelete

.